Kocha Badou: Umefika muda wa Msuva kwenda kucheza Ulaya

Muktasari:

Badou ambaye alipenda kumtumia Msuva katika wachezaji wake watatu wa mbele au wawili kama akitumia 4-4-2, tumepata nafasi ya kufanya naye mazungumzo kwa njia ya mtandao na kufunguka machache kabla ya kuanza majukumu yake mapya.

PANGA pangua ulikuwa huwezi kumwambia kitu Ezzaki Badou (60) akakusikia kuhusu mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva ambaye alikuwa akifanya vizuri katika mfumo wake wa 3-4-3 ambao alikuwa akipenda kuutumia katika klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco.
Kwa sasa mtaalamu huyo wa mbinu za soka amepata kitengo cha kuwa mkurugenzi wa Ufundi, hivyo hakuwa na jinsi zaidi ya kuachana na Difaa kwa kuchangamkia dili hilo la kufanya kazi na Shirikisho la Soka nchini humo.
Badou ambaye alipenda kumtumia Msuva katika wachezaji wake watatu wa mbele au wawili kama akitumia 4-4-2, tumepata nafasi ya kufanya naye mazungumzo kwa njia ya mtandao na kufunguka machache kabla ya kuanza majukumu yake mapya.
Mzaliwa huyo wa Sidi Kacem, Morocco, anasema Msuva ni mshambuliaji bora zaidi wa kigeni ambaye amekuwa akifanya vizuri na klabu hiyo kwa msimu wa tatu sasa tangu atue nchini humo akitokea Tanzania ambako alikuwa akiichezea Yanga.
“Ni miongoni mwa wachezaji bora kwangu wa kigeni. Kwa muda ambao nimekuwa naye tumeshirikiana vizuri, ni mwepesi kuelewa na amekuwa akijitolea kwa kucheza kwa asilimia zote uwanjani bila ya kuwa na hofu ya kupata majeraha,” anasema.
Ndani ya msimu wake wa kwanza Morocco, Msuva aliifungia Difaa jumla ya mabao 14 yakiwemo matatu katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwa mchezaji wa kigeni mwenye mabao mengi zaidi katika ligi ya nchini hiyo maarufu kama Batola Pro.
Mambo yalimwendea tena vizuri msimu uliofuata wa 2018/19 ambapo aliifungia klabu hiyo mabao 13, akivunja rekodi ya msimu wake wa kwanza ambao alipachika mabao 11 katika ligi.
Akikizungumzia kikosi kwa ujumla cha Difaa ambacho amekiacha kama kinaweza kufikia malengo ambayo walijiwekea ya kurejea msimu ujao katika mashindano ya kimataifa, Badou anasema bado nafasi ipo wazi na kwamba, wanatakiwa kuendelea kuipambania.
“Siyo rahisi kumaliza msimu ukiwa katika nafasi tatu za juu, lakini kitu ambacho kinawezekana kama wataendelea kucheza kwa kujituma, naamini nimekiacha kikosi kizuri ambacho kuna maboresho yalikuwa yakitakiwa kufanyika katika maeneo machache.”
Ligi ya Batola Pro imekuwa ikitoa timu nne kushiriki mashindano ya kimataifa, bingwa ambaye huwa ni kinara katika msimamo amekuwa akipata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na aliyeshika nafasi ya pili.
Timu inayomaliza katika nafasi ya tatu imekuwa ikipata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika. Morocco wana nafasi nyingine ya kushiriki michuano ya kimataifa kupitia Kombe la FA nchini humo.
Kwa uwezo ambao ameuonyesha Msuva ambaye msimu huu ana mabao mawili katika ligi mpaka sasa, Badou anasema ni wakati sahihi kwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania kwenda kujaribu bahati yake barani Ulaya.
“Nimekuwa nikisikia kuwa anaweza kuondoka, kwangu taarifa hizo zikiwa rasmi zitakuwa ni habari njema, amekuwa hapa kwa miaka mitatu, sioni kama kuna jambo la kumfanya ashindwe kwenda kwingine kukabiliana na changamoto mpya za soka,” anasema.
Badou ambaye alikuwa kipa, alistaafu soka 1993 akiwa na umri wa miaka 34, ndipo alioamua kusomea ukocha na 2002 alianza kufundisha rasmi na miongoni mwa klabu alizozinoa ni pamoja na FUS na WAC, ambazo aliwahi kuzichezea.
Kocha huyo amemtakia kila la heri Abdelkader Amrani ambaye ameteuliwa kuchukua mikoba yake ndani ya klabu hiyo.
Abdelkader Amrani ni miongoni mwa makocha wenye mafanikio zaidi nchini Algeria, na kwa mujibu wa Badou ni kwamba anaweza kuisaidia Difaa kufanya vizuri nchini Morocco kutokana na uzoefu alionao wa kufundisha soka la ukanda huo.
Miongoni mwa klabu ambazo zimefundishwa na kocha huyo mpya wa kina Msuva na Nickson Kibabage wanaoichezea Difaa ni pamoja na ASO Chlef, USM Alger, USM Blida, USM Annaba, WA Tlemcen, CA Bordj Bou Arréridj, JS Saoura, MO Béjaïa, Al-Raed, CS Constantine na CR Belouizdad.
Kila la heri Msuva katika harakati zako za kusaka maisha bora zaidi ya soka.