Arteta asaka beki mpya Arsenal kila kona

LONDON, ENGLAND. MIKEL Arteta anaamini Arsenal watafanya biashara ya kusajili Januari hii baada ya kikosi chake kuwa na shida kwenye sehemu ya ulinzi.
Jambo hilo linafanya beki wa kati wa RB Leipzig, Dayot Upamecano na Samuel Umtiti wa Barcelona husishwa na mpango wa kwenda kujiunga na wakali hao wa Emirates, sambamba na mabeki wengine wa Juventus, Daniele Rugani na Merih Demiral.
Kocha Arteta amekuwa na wigo finyu wa uchaguzi wa wachezaji wake kwenye sehemu ya mabeki baada ya Rob Holding kuwa na shida nyingi zinazomfanya ashindwe kuwa fiti kwa wakti.
Mabeki wa pembeni Kieran Tierney na Hector Bellerin nao hawatakuwapo kwenye mechi ya leo Jumamosi watakapokipiga na Crystal Palace, huku Arteta akisema kwamba timu yake bado haijatulia kwenye ukuta wake.
Sambamba na hilo, beki Calum Chambers atakuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima baada kupata maumivu ya goti siriazi. Hilo linamfanya kocha Arteta awalazimishe mabosi wake kuingia sokoni Januari hii kufanya usajili.
"Tunafuatilia kwa sababu tumekuwa na majeruhi wengi ambao watakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Tunatazama kama tutakuwa na mchezaji tutakayeweza kumsajili," alisema Arteta.
Kwa muda mrefu, Umtiti amekuwa akihusishwa na mpango wa kutua Arsenal,  huku Upamecano akiibuka na kupewa kipaumbele kwa siku za karibuni, huku dau lake likidaiwa kwamba linaweza kuwa na Pauni 45 milioni.
"Sitarajii kitu kikubwa sana. Natarajia kitu kikubwa kwa wachezaji waliopo hapa, kuna wengine watarudi kutoka kwenye majeruhi, vitu kama hivyo, lakini pia tunanangalia uwezekano wa watu wapya," alisema.