Kisa bao Anfield; Samatta awafunikia Cantona, Ronaldo, Ole Gunner, Aguero

Muktasari:

Wimbo huo ulisikika katika masikio ya Samatta akiwa na KRC Genk, na hata zile kelele ambazo Silvestre alizizungumzia alizisikia, lakini akili ya Samatta ilielekea katika mchezo ndio maana alifunga bao kwenye uwanja huo licha ya kuwa chama lake lilipoteza kwa mabao 2-1 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya

KONGOLE Mbwana Samatta! Mikael Silvestre ambaye katika uchezaji wake soka ametwaa mataji manne akiwa na Machester United aliwahi kusema kwenda Anfield kucheza dhidi ya Majogoo wa Jiji Liverpool ni kama unakwenda kuzimu, maana hakuna wa kukukaribisha na unaweza kuhisi unachukiwa.
Hisia za kuchukiwa zinaweza kukuingia kutokana na vile ngoma za masikio zitakavyokuwa zinapokea kelele za mashabiki wa Liverpool ambao wamekuwa wakipenda kuuimba wimbo wao wa ‘You Will Never Walk Alone’.
Wimbo huo ulisikika katika masikio ya Samatta akiwa na KRC Genk, na hata zile kelele ambazo Silvestre alizizungumzia alizisikia, lakini akili ya Samatta ilielekea katika mchezo ndio maana alifunga bao kwenye uwanja huo licha ya kuwa chama lake lilipoteza kwa mabao 2-1 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hakuna uwanja mgumu pale England kama huo hata Wayne Rooney na Ryan Giggs ambao walitamba wakiwa na Manchester United wamewahi kuuzungumzia ugumu wa kucheza Anfield.
Turudi nyuma hadi Mei 7 ambapo Majogoo hao waliikaribisha FC Barcelona ikiwa na Lionel Messi huku Luis Suarez na Philippe Coutinho wakirejea nyumbani.
Licha ya kuwa na mtaji wa mabao 3-0 waliyoyapata wakiwa Camp Nou katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ndipo kauli ya Silvestre kuwa Uwanja wa Anfield ni kama kuzimu ilitimia kwani FC Barcelona ilijikutaka ikipigwa 4-0 kama imesimama vile huku Messi, Suarez na Coutinho wakishindwa kufunga. Wakati hao wakishindwa kwa Samatta iliwezekana katika usiku huo wa Ulaya. Wafuatao ni mastaa wa Manchester United ambao katika uchezaji wao nchini humo  walishindwa kutupia mabao Anfield.

ERICK CANTONA
Tangu akiwa na Leeds United na hata Manchester United, Cantona hakufunga bao Anfield. Mwaka mmoja kabla ya Manchester United kumsajili, Liverpool ilikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya hivyo. Lakini kocha wa Liverpool wakati huo alimkataa.
Ingawa hakufunga Anfield katika uchezaji wake soka bado alitoa huzuni kwa mashabiki wa Liverpool kwa
kuwafunga bao la dakika ya 86 kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la FA la 1996.

OLE   SOLSKJAER
Kocha wa Manchester United, Ole Gunner Solskjaer enzi zake akiicheza timu hiyo katika michezo 235 na kufunga mabao 91, pamoja na kucheza kwake  kwa mafanikio hakuwahi kupachika bao Anfield.

PAUL  SCHOLES
Scholes ambaye alikuwa hodari katika upigaji wa mashuti, aliichezea United michezo 499 ya Ligi Kuu England akiwa na Mashetani Wekundu wa Old Trafford kati ya 1993 na 2013, akifunga mabao 107.
Katika miaka hiyo 20 alicheza kwenye Uwanja wa Anfield mara 14 katika Ligi Kuu na mara moja Kombe la FA, lakini akashindwa kufunga bao hata moja Anfield.

RUD VAN  NISTELROOY
Tofauti na wachezaji wenzake Solskjaer na Scholes, Nistelrooy hakutumika kwa miaka mingi Old Traford, ambapo ilimchukua misimu matano pekee kutumika klabuni hapo.
Katika misimu hiyo akiwa na Manchester United alifunga mabao 95. Hata hivyo hakuwahi kufunga bao katika michezo mitano ambayo alicheza Anfield, ukiwemo mmoja wa Kombe la FA nchini humo.

CRISTIANO RONALDO
Katika safari zake tano kwenye Uwanja wa Anfield kama mchezaji wa Manchester United, Cristiano Ronaldo ambaye ana tuzo tano za mchezaji bora wa dunia (Ballon d’ Or) sawa na Messi alishindwa  kufunga bao Anfield.