Maajabu Anfield: Liverpool haijapoteza mechi hapo tangu 2017 Manchester United itaweza

Muktasari:

Kwa rekodi hiyo ya Liverpool haijafungwa nyumbani kwenye ligi tangu Aprili 2017 na rekodi ya Man United ya ugenini msimu huu na wameshinda mechi tatu tu kati ya 11, kama watashinda Anfield basi hayo ni maajabu yanayosubiriwa kutokea.

Liverpool, England. MECHI 21 wamecheza. Mechi 20 wameshinda. Mechi moja sare, hawajapoteza mechi yoyote na wavu wao umeguswa mara 14 tu, wakao wao wamegusa nyavu za watu mara 50.
Hayo ndio maajabu ya Liverpool kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Wapo kwenye mchakato wa kuisaka rekodi ya Arsenal ya kucheza msimu mzima bila ya kupoteza mechi kwenye ligi. Wataweza, au kuna maajabu mengine yatatokea?
Kesho huko Anfield, kutapigwa kipute cha maana wakati wenyeji hao Liverpool watawakapowakaribisha mahasimu wao wa siku nyingi, Manchester United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England. Msimu huu, mechi ambayo Liverpool ilipoteza pointi, ilikuwa dhidi ya Man United kwenye raundi ya kwanza ya ligi hiyo.
Sasa wababe hao wa Old Trafford watasimama tena mbele yao wakijaribu kufanya mambo kutibua mwendo wa Liverpool wanaopania kulinyakua taji la Ligi Kuu England msimu huu. Liverpool hawajapoteza mechi, je watafanya hivyo kwenye kipute hicho cha Man United?
Kiwango cha Man United kimekuwa cha kupanda na kushuka, hakieleweki kama homa za vipindi.
Lakini, wamejenga utamaduni unaoogopesha wa kuzibania timu zinazohitaji kutengeneza historia. Hata hivyo, hiyo kesho patakuwa pagumu, kwa sababu Liverpool mara ya mwisho kupoteza mechi uwanjani kwao ilikuwa Aprili 2017. Wasiwasi mwingine ni Man United inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa imekumbwa na majeruhi kibao ya wachezaji wake muhimu, ikiwamo Marcus Rashford, ambaye haieleweki kama atakuwa fiti kucheza.
Kwa rekodi hiyo ya Liverpool haijafungwa nyumbani kwenye ligi tangu Aprili 2017 na rekodi ya Man United ya ugenini msimu huu na wameshinda mechi tatu tu kati ya 11, kama watashinda Anfield basi hayo ni maajabu yanayosubiriwa kutokea.
Man United ya ugenini haina maajabu, mechi hizo 11, imeshinda tatu, sare tatu na kuchapwa mara tano, huku wakiwa wamefunga mabao 12 na kufungwa 15 hivyo wanamiliki hasi ya mabao matatu kwa rekodi zao za nje ya nyumbani kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Wataweza kweli? Lakini, rekodi za jumla, Liverpool wamechapwa mara nyingi na Man United. Kwenye mechi zao zote walizocheza, Liverpool imeshinda mara 76, wakati Man United imeshinda mara 88 na mara 67, timu hizo zilitoka sare. Lakini, kwa miaka ya karibuni, Man United wameshinda mara moja tu dhidi ya wapinzani wao hao. Patamu hapo.
Mara ya mwisho Man United ilipokwenda Anfield ilichapwa 3-1, Jose Mourinho akapoteza ajira yake huko Old Trafford. Je, Ole Gunnar Solskjaer, atachomoka salama uwanjani hapo? Kambi ya Man United ina majeruhi kibao, wote wakiwa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha kwanza kama Scott McTominay (goti), Paul Pogba (mguu), Axel Tuanzebe (paja), Marcos Rojo (ugonjwa), Marcus Rashford (mgongo), Luke Shaw (paja).
Mchezo mwingine wa ligi hiyo utakaopigwa kesho, Burnley watakuwa nyumbani kuwakaribisha Leicester City, ambao wikiendi iliyopita walienguliwa kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.
Mchakamchaka wa ligi hiyo utaendelea leo Jumamosi kwa mechi kibao, ambapo mapema kabisa Mourinho na chama lake jipya la Tottenham Hotspur atakuwa ugenini kwa Watford, wakati Arsenal watakuwa Emirates kuwakabili Sheffield United huku Aston Villa watasafiri hadi kuwakabili Brighton.
Mabingwa watetezi, Manchester City watajimwaga Etihad kucheza na Crystal Palace ya Wilfried Zaha, wakati Bournemouth wao watasafiri hadi kwa Norwich City na Southampton ya mkali Danny Ings itakuwa nyumbani kucheza na Wolves huku David Moyes na West Ham United yake akiwa nyumbani kumkaribisha Carlo Ancelotti na chama lake la Everton huku Chelsea ya Frank Lampard itakuwa ugenini kwa Newcastle United.