Ajax, Inter Milan nje Ligi ya Mabingwa, Liverpool, Barcelona zapeta Uefa

Muktasari:

Presha ilianza kuwapanda Liverpool baada ya timu hiyo inayocheza soka la kuvutia kuwabana hadi dakika ya 56. Lakini Naby Keita na Mohammed Salah walifunfa mabao mawili nfani ya dakika mbili (dakika 57 na 58).

London, England. Inter Milan imeshindwa kwa mara ya pili mfululizo kuvuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kulala 2-1 nyumbani dhidi ya Barcelona, huku bao la ushindi la dakika za lala salama la Ansu Fati likimfanya aweke rekodi ya kuwa mfungaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya michuano hiyo.

Vinara hao wa Serie A walihitaji angalau kufanana matokeo na yale ya Borussia Dortmund dhidi ya Slavia Prague kutokana na kulingana pointi saba kabla ya mechi, lakini Wajerumani hao waliibuka na ushindi wa 2-1 na kusonga mbele huku Inter wakibaki wakijilaumu kwa kupoteza nafasi nyingi.

Baada ya kuvituliza vishindo vya mapema vya Inter, kikosi cha Barca kilichofanyiwa mabadiliko makubwa ya kuchezesha wachezaji wasio wa kikosi cha kwanza, kilitangulia kupata bao kupitia kwa mchezaji wao Carles Perez, ingawa uongozi haukudumu– Romelu Lukaku akikomboa kwa shuti kali la yadi 20.

Lukaku kisha akapoteza nafasi nyingi, ikiwamo nzuri ya mapema kipindi cha pili, kabla ya hatima ya Inter kuamuliwa dakika mne kabla mchezo kumalizika na kinda wa miaka 17, Fati, na kuwashusha Waitalia hao hadi katika Ligi ya Europa.

Ajax ambao msimu uliopita walitisha wakikaribia kwenda fainali kabla ya kutolewa katika nusu fainali na Tottenham kwa magoli ya ugenini, wameaga mapema msimu huu baada ya kulala 2-1 dhidi ya Valencia ambao wameenda hatua ya 16 bora pamoja na Chelsea ambao jana waliifunga Lille 2-1.

Cesar Azpilicueta na Tammy Abraham waliifungia Chelsea magoli yao wakati la kufutia machozi la Lille likifungwa na jyota wa zamani wa Chelsea, Loic Remy.

Lilikuwa ni kundi gumu kwani timu tatu za juu zilitofautiana kwa pointi moja tu. Valencia na Chelsea wamemaliza na pointi 11, lakini timu hiyo ya Hispanis imemaliza kileleni kutokana na rekodi bora ilipocheza dhidi ya Chelsea. Ajax ambayo imeangukia kwenye Ligi ya Europa, imemaliza na pointi 10.

Mabingwa watetezi Liverpool walifuta hofu ya kutolewa mapema kama wangepoteza mchezo wa leo baada ya kushinda 2-0 ugenini dhidi RB Salzburg ya Austria.

Presha ilianza kuwapanda Liverpool baada ya timu hiyo inayocheza soka la kuvutia kuwabana hadi dakika ya 56. Lakini Naby Keita na Mohammed Salah walifunfa mabao mawili nfani ya dakika mbili (dakika 57 na 58).

Liverpool wamemaliza kileleni mwa kundi lao wakiwa na pointi 13 wakifuatwa na Napoli yenye pointi 12 ambayo imeifunga timu ya Mbwana Samata mabao 4-0, shukran kwa hat-tick ya Milik Arkadiusz.

RB Leipzig walitoka sare ya 0-0 dhidi ya wote kutinga hatua ya mtoano huku timu hiyo ya Ujerumani ikimaliza kileleni. Benfica baada ya kuigonga Zenit 3-0 usikuvwa kuamkia leo iliifikia Zenit kwa pointi 7 na kuishusha katika nafasi ya tatu na kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Europa