AFC Leopards 'Ingwe' tuko sawa, kocha mpya ajishasha

Muktasari:

Katika kuhakikisha kwamba wachezaji hawavurugiki mawazo baada ya kusepa kwa kocha Mbungo, Kimani kawakumbusha kuwa sio wao tu wanaopitia hali ngumu ya kifedha hivyo ni lazima  wapambane

KAIMU kocha wa AFC Leopards, Anthony Kimani kaanza vishasha muda tu baada ya menejimenti ya klabu hiyo kumkabidhi kazi hiyo baada ya aliyekuwa kocha wao, Casa Mbungo kujitoa.

Kimani anasisitiza kuwa Ingwe wako tu sawa licha ya kugura kwa Mbungo aliyekuwa mwalimu wao kwa miezi 11.
Kimani sasa anawataka mashabiki wa klabu hiyo wasipaniki akiwasisitizia kwamba naye kaiva kwenye masuala ya ukufunzi hivyo matokeo ya timu hayatanyumba.

Licha ya kuwa wanapitia hali mbaya ya msoto toka walipokimbiwa  na mdhamini, Mbungo kabla hajaondoka alihakikisha kwamba anazalisha matokeo ya kuridhisha. Kaondoka akiwa amesimamia mechi 14 kwenye msimu mpya na kapoteza mara mbili pekee huku akiiwacha timu katika nafasi ya saba.
Sasa Kimani naye kajishasha kuwa yupo na uwezo wa kuendeleza matokeo hayo hivyo mashabiki hawapaswi kupaniki.
“Bosi kaondoka na namshukuru sana kwa kunisaidia kuanza taaluma yangu kama mkufunzi. Kanifunza mengi, ni machungu kuona akiondoka ila hamna tunachoweza kufanya zaidi ya kuendelea na kasi aliyotuacha nayo. Jumapili tuna mechi na sioni sababu ya kutuzuia kuendelea kufanya vizuri,” Kimani aliyebeba taji la ligi kuu akiwa mchezaji 2008 na Mathare United kasema.
Katika kuhakikisha kwamba wachezaji hawavurugiki mawazo baada ya kusepa kwa kocha Mbungo, Kimani kawakumbusha kuwa sio wao tu wanaopitia hali ngumu ya kifedha hivyo ni lazima  wapambane.
“Tuna matatizo ya kifedha ila ukiangaliza vizuri sio sisi tu. Pia zipo timu kadhaa zinateseka na licha ya hali hiyo, zinaendelea kujitahidi, nasi tunapaswa kuendelea hivyo,” Kimani kaongeza.
Katika mechi tano za mwisho walizocheza, Ingwe hawajapoteza mechi hata moja wakishinda mbili na kutoka sare tatu.