Yusuf Mhilu anazidi kuzifumania nyavu Kagera Sugar yapaa

Muktasari:

Mhilu amefunga bao hilo wakati klabu yake ya Kagera Sugar ilipoichapa Mbao FC mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

KASI ya ufungaji ya mshambuliaji wa Kagera Sugar, Yusuf Mhilu, imekuwa tishio kwa straika na kinara wa mabao wa Simba na Ligi Kuu Bara, Mnyarwanda Meddie Kagere katika kuwania kiatu cha ufungaji bora msimu huu.
Hii ni baada ya kupachika bao la tisa na kumfanya Kagere mwenye mabao 12, amzidi matatu tu.
Mhilu amefunga bao hilo wakati klabu yake ya Kagera Sugar ilipoichapa Mbao FC mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera. Mshambuliaji huyo alifunga dakika ya 31, baada ya Geofrey Mwashiuya aliyepachika dakika ya nane.
Mhilu anashika nafasi ya pili sawa na Reliants Lusajo wa Namungo FC wakiwa na mabao tisa, baada ya Kagere mwenye 12. Paul Nonga, Daruwesh Saliboko wote wa Lipuli FC na Mzambia Obrey Chirwa wa Azam FC wanashika nafasi ya tatu kila mmoja amefunga mabao manane.
Kagere ndiye mfungaji bora wa msimu uliopita na alifunga mabao 23.

SINGIDA UNITED SHIMONI
Inawezekana pale mkiani kuna raha yake. Singida United wameendelea kung’ang’ania mkiani  mwa msimamo wa ligi baada ya kufungwa nyumbani kwao Uwanja wa Liti na Ndanda FC bao 1-0 mfungaji akiwa Vitalis Mayanga dakika ya 80, huku KMC FC imechapwa na Polisi Tanzania mabao 3-2 kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Uhuru, mechi iliyopigwa saa 8:00 mchana.
Ruvu Shooting wameipiga Mbeya City bao 1-0 lililopachikwa na Fully Maganga dakika ya 50. Biashara United wao walitamba kwao kwa kuifunga Alliance FC bao 1-0 likipachikwa na Okorie James katika dakika za nyongeza baada ya 45 kumalizika.
Kikosi cha Mtibwa Sugar kimepigwa kwao Gairo na JKT Tanzania bao 1-0 mfungaji akiwa Danny Lyanga kwa njia ya penalti dakika ya 33.
Mwadui FC wamelazimisha sare ya 1-1 na Namungo FC, mabao yakifungwa na Nzigamasabo Steve kwa Namungo dakika ya nane na Raphael Aloba kuisawazishia Mwadui dakika ya 49.