Yondani aonyesha ubora wake akicheza nafasi ya kiungo mkabaji

Muktasari:

Kocha wa Yanga Mbelgiji, Luc Eymael amepanga, beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani kucheza kiungo badala ya beki wa kati.

Dar es Salaam. Beki Kelvin Yondani 'Vidic' ameonyesha uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji leo wakati timu yake ikicheza dhidi ya Gwambina FC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Yondani kwa takribani miaka 15 amekuwa akicheza nafasi ya beki wa kati, lakini leo kocha Luc Eymael aliamua kumchezesha nafasi ya kiungo mkabaji.

Yondani alicheza nafasi hiyo vizuri akisaidia ulinzi huku akiwa na maelewano mazuri na Haruna Niyonzima katika eneo la kiungo la Yanga.

Tangu Eymael ametua Yanga, Yondani amepoteza nafasi katika kikosi cha kwanza mara kadhaa amekuwa akiweka benchi au kuingia akitokea benchi.

Hata hivyo Yondani alitolewa katika kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Sonso wakati huo Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.