Jicho la Mwewe: Tatizo ni wachezaji wa kigeni au sisi wenyewe?

Muktasari:

Napata shida kuamini kama tungefikiria kuleta wachezaji wa kigeni katika kikosi ambacho kina Hussein Marsha, Hamis Gaga, Athuman China na Ally Maumba. Mgeni angecheza nafasi ya nani hapo? Hakuna.

NILIMSIKIA waziri mwenye dhamana katika mchezo wetu akifikiria kupunguza wachezaji wa kigeni nchini kufikia watano kwa kila klabu. Ni kitu kinachofikirisha. Lakini hata hivyo limekuwa suala la kisiasa na matakwa binafsi ya mwenye dhamana.
Kuna watu wanaingia pale TFF hawataki idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni. Kuna wakati wanaingia watu wanafungua milango. Vigogo wakubwa Simba, Yanga na Azam wana uwezo wa kuwa na wachezaji wengi wa kigeni ndio ambao wanayumbisha watu wenye dhamana.
Achana na hilo. Turudi katika ukweli. Kiini cha tatizo nini? Wachezaji wa kigeni au wachezaji wetu? Vyote viwili. Inawezekana waziri mwenye dhamana yake anashawishika kwa sababu anaona kuna wachezaji wengi wa kigeni ambao ni wabovu. Hili tatizo lipo.
Lakini hapo hapo tuulizane. Ni kweli wachezaji wetu wana viwango vizuri kiasi hatuhitaji wachezaji wa kigeni katika maeneo mengi uwanjani? Sio kweli. Wachezaji wa kileo ndio ambao wanasababisha tuvamie masoko ya nje na kujaribu wachezaji wan je.
Napata shida kuamini kama tungefikiria kuleta wachezaji wa kigeni katika kikosi ambacho kina Hussein Marsha, Hamis Gaga, Athuman China na Ally Maumba. Mgeni angecheza nafasi ya nani hapo? Hakuna. Mgeni anachezaje katika nafasi ya Mohamed Hussein au Edibily Lunyamila? Mgeni anapataje nafasi katika kikosi chenye Malota Soma na Edward Chumila?
Tukubaliane tuna wachezaji wengi wenye viwango vya kawaida katika miaka ya karibuni. Vipaji bado vipo, lakini havichezi kwa asilimia 100 ya uwezo wao na ndio maana labda wenye fedha wanaona umuhimu wa kuleta wageni.
Hata hivyo, kuna mambo mawili yanajitokeza katika mchakato wa kuleta wageni. Kwanza kabisa tunaongozwa na watu ambao sio wataalamu katika masuala ya soka. Hawajui nafasi ya kufanya utafiti kabla ya kumchukua mchezaji wa kigeni. Kifupi tunaweza kuita ‘scouting’. Bado ni duni.
Kuna watu wanatumia mwanya huo katika kujinufaisha. Wanaangalia wanapata nini katika uhamisho huo. Wakati mwingine hawaangalii sana kiwango cha mchezaji. Hapa ndipo wanapochanganya mchele na pumba. Wakati mwingine wanaleta mchezaji ambaye ambaye anaweza kupatikana nchini.
Wakati mwingine watu hawa ambao hawana maarifa sana na soka huwa wanachukua wachezaji wa kigeni kwa fasheni. Mara nyingi wanaangalia nje ya mipaka kwa sababu wakubwa wenzao wamefanya hivyo. Basi.
Katika hali ya kawaida mchezaji ambaye anatoka nje ya nchi inabidi awe na mambo tofauti zaidi kuja kucheza nchi ya dunia ya tatu ambayo tunachukulia kwa haraka haraka kwamba klabu yake ni maskini na imeamua kumfuata kwa sababu ina uhitaji mkubwa wa mchezaji wa aina yake na haimchukui kama fasheni.
Hapo bado wakubwa wanaboronga. Hawaangalia umaskini wa klabu yao. Jaribu kuangalia jinsi ambayo Yanga ilikuwa ‘ikiungaunga’ katika miaka ya karibuni, huku wachezaji wakikosa mishahara. Ungetegemea kwamba wangekuwa makini kuhakikisha kama wanachukua mchezaji wa kigeni basi awe bora na wasipoteze pesa zao. Bado wamemchukua mchezaji kutoka Ivory Coast ambaye anaonekana wazi hana uwezo mkubwa uwanjani.
Hili suala la kwamba wachezaji wa kigeni wanaokuja nchini, lazima wawe wanachezea timu zao za taifa silipi uzito sana. Unaweza kupata mchezaji mzuri kutoka Ghana, Ivory Coast, Mali, Senegal na kwingineko na asiwe katika timu yake ya taifa. Ni ngumu kucheza Afrika na kuingia katika vikosi vya timu hizi za taifa.
Kuna mastaa kibao wa nchi hizi ambao wanacheza katika Ligi Kubwa Afrika na klabu kubwa kama Zamalek, TP Mazembe, Etoile du Sahil, Al Ahly na wengineo lakini hawafikiriwi kuitwa katika vikosi vyao vya timu za taifa. Ni hoja hafifu.
Mwisho wa siku hili ni suala lenye utata mwingi ndani yake. Waingereza waliamua ligi yao iwe bora na kuruhusu wachezaji wengi wa kigeni katika. Sisi tuliruhusu hili, lakini imekuwa bahati nasibu. Wakati mwingine tunaambulia magalasa wakati mwingine tunaambulia wachezaji wa ukweli kama kina Thabani Kamusoko, Kipre Tchetche, Emmanuel Okwi na wachache wengineo.
Vyovyote ilivyo wachezaji wetu ndio wameruhusu hali hii ya viongozi wao wakati mwingine kuleta wachezaji wa kigeni walio wazuri au magalasa.
Kama wangekuwa wanajikuta, kwa vipaji walivyonavyo, sidhani kama wachezaji wa kigeni wangekuwa wanaingia nchini kiholela.