Twiga Stars kuivaa Algeria, Tunisia mchana huu

Muktasari:

Kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ya Twiga Stars, kitacheza mechi yake ya pili nchini Tunisia dhidi ya Algeria katika michuano ya Kram.

Dar es Salaam.Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya ya soka ya wanawake inayosimamiwa na Shirikisho ka Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Kaskazini (UNAF), Twiga Stars leo Jumapili saa 8;00 mchana itakuwa kibaruani dhidi ya Algeria.

Twiga Stars itacheza mchezo huo kwenye Uwanja wa Kram uliopo, Tunis, Tunisia ukiwa wa pili baada ya wa kwanza kuichapa Mauritania mabao 7-0, mechi ya kwanza.

Baada ya mchezo huo, wenyeji Tunisia watakipiga na Mauritania majira ya saa 10: 30 katika uwanja huo wa Kram.

Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime 'Mchawi Mweusi' amesema, wako tayari kwa mchezo huo.

"Kila kitu kipo vizuri tayari kwa mchezo huo. Kiujumla naifurahia michuano hiyo kwa sababu itatusaidia katika safari yetu ya michuano mikubwa iliyo mbele yetu," alisema Shime kocha aliyewahi kuzinoa timu za JKT Tanzania na Coastal Union ya Tanga.

Jumla ya mataifa matano yameshiriki katika michuano hiyo ambayo ni Tanzania waalikwa, Algeria, Mauritania, Morocco na wenyeji Tunisia.