Poulsen anamfuata Samatta Ligi Kuu England

Muktasari:

Kwa mujibu wa ripoti, nyota wa RB Leipzig, Yussuf Poulsen yupo kwenye rada za Newcastle United

STRAIKA wa RB Leipzig ya Ujerumani, Yussuf Poulsen, 25, mwenye asili ya Tanzania ameripotiwa kuwindwa na klabu ya Newcastle United inayoshiriki Ligi Kuu England ikiwa ni mpango wa kuongeza makali kwenye safu yao ya ushambuliaji.
Vyanzo mbalimbali vya habari vya Kiingereza, vimeripoti kuwa Newcastle United wapo kwenye nafasi nzuri ya kumsajili nyota huyo ambaye amepoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha RB Leipzig.
Nyota huyo ambaye asili yake ni mtu wa Tanga (Mdigo), alijiunga na RB Leipzig, Julai 2013 akitokea Lyngby BK ya Denmark ambako alisajiliwa kwa ada ya uhamisho wa Euro 1.55 milioni. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2022.
“Kwa mujibu wa ripoti, nyota wa RB Leipzig, Yussuf Poulsen yupo kwenye rada za Newcastle United,” gazeti la The Evening Chronicle liliandika likieleza kuwa mshambuliaji huyo anatazamwa kama chaguo la kwanza la Newcastle.
Msimu huu, Poulsen amefunga mabao matatu na kuasissti mabao matano katika michezo 20 aliyoichezea klabu yake kwenye Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’.
Poulsen ambaye amekuwa akitumika katika kikosi cha timu ya taifa ya Denmark na alifunga bao katika fainali za Kombe la Dunia nchini Ufaransa 2018, huu ni msimu wake wa sita kucheza Bundesliga na msimu uliopita alikuwa katika kiwango cha juu zaidi akifunga mabao 19 katika mechi 25.
Kwa sasa anayeonekana kuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji ya klabu yake ni Timo Werner.

MSIMAMO WA POULSEN
Poulsen anaamini bado ana nafasi ya kuendelea kucheza kikosi cha kwanza cha RB Leipzig licha ya kuwa ndoto yake siku moja ni kucheza Ligi Kuu England.
“Mimi ni kama askari hivyo niwapo vitani ni wajibu wangu kuendelea na mapambano,” alisema mshambuliaji huyo.
Akizungumzia kuhusu kucheza Ligi Kuu England, alisema, “Ni moja ya Ligi ambazo kila mchezaji amekuwa na ndoto ya kucheza, tusubiri wakati sahihi utakapofika pengine inaweza kutokea.”
Akitua, ataungana na Mtanzania Mbwana Samatta anayekiwasha katika Ligi Kuu ya England akiwa na Aston Villa.