Kihwelo ‘Julio’: Bila ya mimi Mkude asingekuwepo Simba

Muktasari:

Jonas Mkude ni mmoja wa wachezaji aliyedumu muda mrefu ndani ya klabu ya Simba pamoja na mara kwa mara kusumbuliwa na tatizo la utovu wa nidhamu

Dar es Salaam. Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ anasema kama si yeye huenda Jonas Mkude asingekuwepo katika ramani ya soka ya Tanzania kwa sasa.

Kiungo Mkude amekuwa akiandamwa na kashfa za mara kwa mara za utovu wa nidhamu, lakini ni moja ya wachezaji waliodumu kwa muda mrefu katika kikosi cha Simba.

Julio anasema bila ya yeye kuwa na msimamo na kutambua uwezo wake huenda asingekuwepo katika ramani ya soka hivi sasa.

Julio alisema, wakati akiwa Kocha wa Simba akifanya kazi na Mfaransa Patrick Liewg hakuwahi kumkubali nyota huyo hivyo yeye ndiye alikuwa shinikizo la kiungo huyo kupata namba ndani ya kikosi hicho.

"Bila ya mimi Mkude sijui angekuwa wapi hivi sasa, huenda hata katika mpira angekuwa asisiki, kwani yule kocha Mfaransa alikuwa hamkubali hata kidogo, yaani hamtaki kabisa, mimi nilikuwa nalazimisha sana mpaka Mkude huyu mnayemuona hivi sasa."

Anasema wachezaji wengine wanapoteza viwango vyao kutokana na falsafa za kila mwalimu ndani ya timu, huku akimtolea mfano Said Ndemla na Ibrahim Ajibu kutoka nafasi ndani ya timu.

"Hao ni wachezaji wazuri, lakini kila mwalimu ana falsafa yake katika timu yake hivyo unakuta mchezaji anashindwa kuendana nazo na kujikuta kiwango chake kufa," anasema Julio.