Mjadala wa nani bora Gerrard, Lampard na Scholes wafungwa

Thursday March 26 2020

Mwanaspoti, Tanzania, England, Mjadala wa nani bora Gerrard, Lampard na Scholes wafungwa

 

LONDON,  ENGLAND. VIUNGO watatu wa Kiingereza. Steven Gerrard, Frank Lampard na Paul Scholes wote walikuwa wababe sana ndani ya uwanja.
Hakuna ambaye hakuona ubora wa mastaa hao wakati walipokuwa wakitamba na timu zao kwenye Ligi Kuu England.
Wakali hao walitamba kwenye Ligi Kuu England (EPL) na timu zao za Liverpool, Chelsea na Manchester United mtawalia.
Lakini, nani alikuwa bora kati ya watatu hao? Swali hilo limekuwa likizua mjadala mzito miongoni mwa mashabiki wa mchezo wa soka, hasa kwa wale ambao wamekuwa wakifuatilia mikikimikiki ya Ligi Kuu England.
Katika kumaliza utata wa jambo hilo, mastaa wenye majina makubwa duniani walihusishwa kwenye mjadala huo kutoa maoni yao juu ya mchezaji gani kwenye orodha ya viungo hao watatu alikuwa bora ndani ya uwanja kuliko wenzake.
Haya hapa ni majibu ya mastaa waliohojiwa kwenye mjadala huo kumtaja mchezaji gani wanadhani alikuwa moto. Wakali hao wote walikuwa Waingereza na walitamba na timu yao ya taifa ya England.
Hata hivyo, maoni ya wachezaji walionekana kutoa kwa mapenzi yao yamewekwa kando kwenye mjadala huo.
Kwa mfano, Jamie Carragher na Michael Owen wote walimchagua Gerrard, huku jambo hilo likidaiwa kwamba kuchangiwa zaidi kwa sababu watu hao walikuwa wakicheza pamoja klabuni Liverpool.
John Terry alimchagua Lampard, wakati Gary Neville alimchagua Scholes, ambapo wakali hao wote wachezaji waliowachagua kuwa ni bora waliwahi kucheza nao timu moja, Chelsea na Manchester United.
Haya hapa ndio majibu ya wanasoka ambao hawakuonyesha upendeleo kwenye kuchagua mchezaji gani bora baina ya wakali hao watatu, viungo wa zamani wa mpira. Mastaa 11 waliotoa majibu yao kwenye mjadala huo, huku kila mmoja akiwa na chaguo lake.

Toni Kroos - Paul Scholes
Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ujerumani, Toni Kroos aliulizwa swali hilo na jibu lake alilotoa mwaka 2017, kuwa kwake mchezaji bora zaidi ya wengine alikuwa Scholes. Kwa bahati mbaya, Kroos hakutoa maelezo ya uchaguzi wake kwa Scholes, lakini wengi hawakusumbua vichwa sana kwa sababu ya kufananisha staili zao za kiuchezaji wawili hao kuwa zimekuwa zikifanana. Pengine, Kroos alimchagua mchezaji anayefanana naye kwenye staili ya kiuchezaji.

Kaka - Steven Gerrard
Kiungo wa Kibrazili, Ricardo Kaka amemchagua Gerrard, ikiwa aliwahi kumenyana naye kwenye mechi za fainali ya Ligi ya Mabinngwa Ulaya mwaka 2005 na 2007, ambapo timu zao AC Milan na Liverpool zilipomenyana. Kaka amecheza dhidi ya wachezaji wengi, lakini anamtazama Gerrard kuwa ni mchezaji aliyekuwa bora zaidi ya wengine kwenye orodha hiyo ya wanaoshindanishwa. “Nampenda Gerrard,” alisema Kaka na kuongeza. “Hii ni kwa sababu tulikuwa na ushindani mkali kwenye fainali 2005 na 2007, namkubali sana. Ndio, Lampard ni mzuri na Scholes ni mahiri, lakini mimi chaguo langu ni Gerrard.”


Thierry Henry - Paul Scholes
Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry alicheza dhidi ya wachezaji wote hao watatu, lakini lilipokuja suala la kumtaja nani mkali kwenye mjadala huo, jibu lake lilikuwa Scholes. Henry, ambaye ni moja kati ya wachezaji mahiri kabisa waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England alisema kuhusu Scholes: “Alikuwa juu ya akili yake. “Aliifanya Man United mambo yake kutiki uwanjani. Kila wakati tulipowakabili Man United basi nilikuwa natafuta namna ya kumfanya adhibitiwe. Sawa ni kweli, Stevie G anaweza kumkaribia, lakini Paul Scholes ni mshindi kwenye hili.”

Deco - Paul Scholes
Fundi wa mpira wa zamani huko Ureno aliyewahi kutamba Barcelona na Chelsea, Deco chaguo lake la moja kwa moja lilikuwa Scholes. Deco alicheza na Lampard kwenye kikosi cha Chelsea kwa misimu miwili, lakini hakutaka kuleta ushabiki lilipokuja suala la kumtaja mchezaji gani anayedhani kuwa ni bora kwenye orodha hiyo, akamtosa mchezaji mwenzake wa zamani huko Stamford Bridge na kumchagua mpinzani, Scholes. Deco alisema: “Nilicheza dhidi ya wachezaji wengi sana kwenye sehemu ya kiungo akiwamo Gerrard. Nilipata pia nafasi ya kucheza na Lampard pamoja huko Chelsea. Lakini, kwa kusema ukweli, Paul Scholes alikuwa kiungo tofauti na wengine huko England. Alikuwa bora, hakika ni mmoja wa wachezaji bora duniani.”

Kieron Dyer - Paul Scholes
Staa Kieron Dyer aliyetamba kwenye Ligi Kuu England kwa misimu 14 kati ya 1999 na 2013, hakutaka kueleza sana, chaguo lake ni Scholes tu.
“Mchezaji bora niliwahi kucheza naye ni Paul Scholes,” alisema Dyer alipozungumza na Soccer AM. “Mjadala siku zote umekuwa nani bora kati ya Scholes, Frank Lampard na Steven Gerrard. Kwa upande wangu, naona Scholes alikuwa bora zaidi yao.
“Watu waliocheza naye timu moja na hata waliowahi kukabiliana naye wanalifahamu hilo vizuri jinsi alivyokuwa spesho na wa kipekee. Alikuwa akifanya kila kitu ndani ya uwanja isipokuwa kupiga ‘tako’ tu!”

Chris Sutton- Steven Gerrard
Fowadi wa zamani, Chris Sutton aliulizwa swali la kuhusu viungo hao watatu nna Robbie Savage kwenye BT Sport. Fowadi huyo hakuwa na mbwembwe nyingi na kumchagua tu Gerrard, akisema ndiye mchezaji bora kwake kwa kumlinganisha na Scholes na Lampard.
Sutton alisema: “Ni swali gumu sana, lakini mimi nitasema bora kati yao ni Gerrard. “Nadhani alikuwa bora kwenye idara zote. Kwenye uwezo wake wa pasi. Ni jambo gumu, lakini chaguo langu mimi ni Gerrard.”

Paul Ince - Paul Scholes
Kiungo wa zamani, Paul Ince yeye aliwahi kucheza na Scholes klabuni Manchester United na Gerrard huko Liverpool. Lakini hakuwa na maneno ya kusitasita wakati alipoulizwa na Savage kwenye BT Sport kumchagua nani bora baina ya wawili hao sambamba na Lampard.
Ince alisema: “Scholes muda wote. Jamaa alikuwa anapiga pasi balaa. Alikuwa na kila kitu kwa kusema haki.”

Bryan Robson- Steven Gerrard
Bryan Robson, gwiji wa Man United hakutaka kuleta ushabiki kwenye mjadala huo naye alimchagua Gerrard mbele ya Scholes.
“Kwa upande wangu Gerrard aliweza kufanya kila kitu na ndio maana namwona ni bora kwenye orodha ya watatu hao. Yeye ni wa kwanza kisha Scholes halafu ndio Lampard kwa kufuata mpangilio huo,” alisema Robson alipohojiwa na Daily Mail mwaka 2013.
“Alikuwa mchezaji wa kiwango cha juu na bora kila idara, ambapo Gerrard alikuwa akipiga ‘tako’, anakaba, anafunga mabao, anapiga vichwa, anapiga pasi na amekuwa na nguvu na kasi. Alikuwa juu sana kwenye soka lake.”

Ruben Loftus-Cheek - Steven Gerrard
Jibu la Loftus-Cheek pengine litamweka kwenye wakati mgumu kwa sasa. Staa huyo wa Chelsea, Loftus-Cheek aliulizwa swali hilo Desemba 2017, lakini kitu kilichoshangaza hakumchagua Lampard, ambaye kwa sasa ni kocha wake huko Stamford Bridge. Chaguo la mchezaji huyo lilikuwa Steven Gerrard.
“Nadhani mimi nitasema Gerrard, kwa sababu ana uwezo wa kufanya kila kitu,” alisema Loftus-Cheek alipozungumza na Metro.
“Sawa, Lampard alikuwa bora kwenye kile alichokuwa akikifanya, kwamba alikuwa akifunga mabao, lakini kwa kumlinganisha na viungo wengine nadhani Gerrard ni bora zaidi.”

WilfrIed Zaha - Steven Gerrard
Winga wa Crystal Palace, Wilfried Zaha aliitumikia Man United kwa muda mfupi, lakini jambo hilo halijamshawishi kumchagua Scholes.
“Binafsi namchagua Gerrard,” alisema Zaha alipozungumza na 90min.com. “Hayo ndio maoni yangu, kwa jinsi tu alivyokuwa akicheza, anamiliki mchezo, mbunifu na anapiga mashuti.
“Nakumbuka kwenye mazoezi ya England, alipiga mpira kwa nguvu sana.”

Robbie Savage - Steven Gerrard
Kiungo mkorofi, Robbie Savage alikulia kwenye timu moja na Scholes klabuni Man United. Lakini, chaguo lake ni Gerrard.
“Nilicheza dhidi ya Scholes, Keane, Vieira, Makelele, Lampard – moja ya viungo bora kabisa kwenye Ligi Kuu England – lakini kwa upande wangu Steven Gerrard alikuwa juu yao,” alisema hilo mwaka 2016.
“Alikuwa na uwezo wa kupiga pasi mita 50, 60. Anapiga ‘tako’, anapiga friikiki, anaweza kufunga mabao, hakika alikuwa balaa kwelikweli uwanjani. Kwangu mimi alikuwa mchezaji bora zaidi huko Liverpool.”

Matokeo ya jumla:
Steven Gerrard – kura 6
Paul Scholes – kura 5
Frank Lampard – kura 0
Kwenye orodha hiyo ya mastaa wa zamani waliochaguo kwa kutoweka ushabiki, Gerrard ametajwa mara nyingi na kuwapiku wenzake.
Lakini, kitu cha kushangaza zaidi, hakuna hata mmoja kwenye mastaa hao 11 aliyemchagua Lampard kuwa mchezaji bora mbele ya viungo wenzake hao wawili waliotamba pamoja kwenye Ligi Kuu England.
Lampard anatajwa kama mchezaji bora zaidi wa nyakati zote Chelsea, ambapo alifunga mabao 177 akitokea kwenye sehemu ya kiungo. Lakini utashangaa hata Deco aliyecheza naye timu moja hakuthaminisha ubora wake, ukimweka kando Loftus-Cheek ambaye amekuwa kwenye timu ya Chelsea tangu alipokuwa na umri wa miaka minane. Hivyo ndivyo mjadala ulivyofungwa, lakini yote kwa yote kila mchezaji alikuwa na ubora wake uwanjani.

Advertisement