Chid Mapenzi alilia penzi la Shamsa Ford

Muktasari:

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Chid Mapenzi  ameweka ujumbe mzito kwa kueleza kuwa hatakuwa wa kwanza kulia kwenye mapenzi na anashindwa kujizua kumkumbuka Shamsa

Wakati mwingine umuhimu wa mtu huonekana pale ambapo unampoteza, hiki ndicho kinachomtokea mfanyabiashara wa mavazi Rashid Said 'Chid Mapenzi', baada ya kuachana na aliyekuwa mke wake Shamsa Ford.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Chid Mapenzi  ameweka ujumbe mzito kwa kueleza kuwa hatakuwa wa kwanza kulia kwenye mapenzi na anashindwa kujizua kumkumbuka Shamsa.
"Sitokuwa wa kwanza kulia kwenye mapenzi, nakukumbuka Shamsa nashindwa kujizuia vyote ulivyokuwa unanikataza kwa faida yangu mwenyewe ndiyo sasa hivi naviona, popote ulipo naomba ujue nakukumbuka sana mama, sina mtu wa kunipa moyo, sina rafiki kama wewe, wewe ndiyo siri wangu, nakukumbuka mama na familia ni kila kitu dah" ameandika Chid Mapenzi.
Baada ya andiko hilo la Chid Mapenzi, Mwanaspoti Online  lilimtafuta Shamsa ili kujua kama ameona ujumbe aliotumiwa na aliyekuwa mume wake huyo.
"Nimeona alichoandika Chid, ila siwezi kujibu kitu kwasasa kwani sina jibu la haraka haraka kiasi hicho na hasa kupitia mtandao au kwenye vyombo vya habari, ila nitakapokuwa tayari kumjibu nitakupigia simu kukwambia, rafiki yangu usihofi"
Wakati huo huo aliyewahi kuwa mpenzi wa Shamsa, mwanamuziki Ney wa Mitego akiweka picha ya mrembo huyo kwenye akaunti yake ya Instagram na kuandika maneno haya:
"Cousin wanasema samehe saba mara 70 . Tafadhali msamehe mwenziooo amekiri makosa, ebu rudi kwa mumeo bana. Tafadhali tafadhali rudi kwa mumeo"
Siku ya pili ambayo ni jana Jumatatu, Machi 30 baada ya andiko Chid Mapenzi , Shamsa kwenye akaunti yake ya Instagram alionekana akituma kipande cha video  akicheza muziki huku akicheka daada ya saa kadhaa ile video haikuonekana na matokeo yake Shamsa alidai video imefutwa.
Baada ya muda aliweka kipande kingine cha video yake, hapo ndipo alipata komenti nyingi kutoka kwa watu akubali msamaha wa Chidi na wengine kumsema amefurahia kuombwa msamaha hadharani huku akiambiwa alikuwa na umuhimu hivyo aache kucharuka na kupotezea ujumbe aliotumiwa.
Leo Jumanne, Mwanaspoti Online lilizungumza na Chid Mapenzi kujua nini kilipelekea hadi kufikia hatua ya kumwandikia ujumbe Shamsa kwenye mtandao wa kijamii wakati anapoishi au namba ya simu anayo? Haya ndio majibu yake
"We acha tu ndugu yangu, bado nampenda mke wangu Shamsa wewe unajua hili, nishamwambia sana kwenye simu na hata kuongea nae uso kwa uso lakini ananiitikia amenielewa ila sioni kurudi, mara ya mwisho uliona na ukashuhudia nilichomwambia lakini ndio hivyo, ndio maana nimeona nitumie njia ya mtandaoni huenda akanielewa zaidi" alisema Chid Mapenzi.
Mwaka 2016, Shamsa aliolewa na Chidi ambaye ni mfanyabiashara ambapo ndoa yao ilikuwa gumzo kwani kabla ya hapo, mrembo huyo alikuwa kwenye uchumba wa muda mrefu na mwanaume aliyefahamika kwa jina la Dickson Matoke ambaye alizaa naye mtoto mmoja wa kiume, Terry.
Mwaka jana, ndoa ya Shamsa na Chid ilivunjika na hawakuwahi kupata mtoto.