Banda tuombeeni hali si shwari kabisa Sauzi

Muktasari:

Beki huyo wa Highlands Park inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini, anasema alianza kusumbuliwa na mafua ya kawaida kabla ya kushikwa na homa, “Niliingiwa na hofu kwa sababu hizo ni miongoni mwa dalili za virusi vya Corona

HOFU  ilizuka kwa wadau na mashabiki mbalimbali  wa soka la Tanzania kutokana na uvumi uliozagaa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Abdi Banda ambaye anaichezea Highlands Park ya Afrika Kusini kuwa  ameambukizwa virusi vya Corona.
Uvumi huo ulivifanya vyombo  vya habari nchini Tanzania  kuhaha kutafuta ukweli  wa taarifa hizo, wakati ambao maambukizi  ya ugonjwa wa virusi vya Corona yalikuwa yameshika kasi Afrika Kusini.
Idadi ya watu waliokuwa wakihusishwa na ugonjwa huo ilikuwa ikiongezeka kila uchao hivyo ilikuwa rahisi kwa wadau na mashabiki wengi wa soka la Tanzania kuingiwa na hofu kuhusu afya ya mchezaji huyo.
Banda  ambaye aliwahi kutamba kwenye Ligi Kuu ya Bara akiwa na klabu ya  Simba na Coastal Union, anasimulia mkasa mzima ulivyokuwa kuanzia dalili alizokuwa nazo, mchakato wa vipimo ulivyochukua nafasi  huku akiwa ametengwa na akaweka namna alivyopokea majibu.
Beki huyo wa Highlands Park inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini, anasema alianza kusumbuliwa na mafua ya kawaida kabla ya kushikwa na homa, “Niliingiwa na hofu kwa sababu hizo ni miongoni mwa dalili za virusi vya Corona.
“Ulikuwa ni wakati mgumu lakini kwa bahati nzuri  viongozi, mashabiki wa klabu yangu ya Highlands na Watanzania walikuwa upande wangu, dalili hizo ziliwafanya wachukue vipimo ili kuona kinachonisumbua,” anasema.
Wakati akisubiri majibu yake, Banda anasema  alikuwa akiomba dua ili asikutwe na maambukizi ya virusi vya Corona wakati huo Afrika Kusini zilikuwa zikinyesha mvua.
“Nilikuwa nikihisi baridi kutokana na hali ya hewa. Niliendelea na maisha mengine nikiwa nyumbani licha ya kuwa wenzangu walikuwa wakiendelea kucheza Ligi kabla ya kusimamishwa wiki chache baadaye,” anasema.
Baada ya siku chache Banda alitaarifiwa kuwa majibu yake yalikuwa tayari. Anasema presha ilikuwa ikipanda na kushuka, lakini kwa bahati nzuri hakukutwa na virusi vya Corona lakini alitakiwa kuendelea kupumzika nyumbani.
“Nipo nyumbani na kama vile ambavyo mnajua. Huku hali sio shwari, kila mtu anatakiwa kukaa  ndani hakuna shughuli zozote zinazoendelea,” anasema.
Jeshi la ulinzi na usalama la Afrika Kusini lilianza Ijumaa ya wiki iliyopita kusimamia utekelezwaji wa amri iliyotolewa na Rais Cyril Ramaphosa ya kila mtu kubaki ndani kwake siku 21 ikiwa ni hatua ya kupambana na kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Mapema kabla ya kuanza kutekelezwa kwa agizo hilo foleni ndefu ya watu ilionekana kwenye maduka makubwa wakifanya manunuzi muhimu ili kujiwekea akiba wakati huu ambao ukikutwa nje unashikishwa adabu na watu wa usalama.
“Binafsi nilinunua mahitaji muhimu mapema kwa hiyo sitakuwa na sababu ya kutoka nje na nimekuwa nikihamasisha marafiki zangu kuhakikisha sote kwa pamoja tunatekeleza agizo la Serikali,” anasema beki huyo wa kati kwenye uwezo wa kucheza pia pembeni na kiungo mkabaji.
Afrika Kusini imeripoti kuwa na wagonjwa ya 1,000 ikiwa ni idadi kubwa zaidi barani Afrika.
Jioni siku ya Alhamisi Rais Cyril Ramaphosa alitembelea kambi ya jeshi kabla askari hao kuruhusiwa kuingia barabarani
“Ninawatuma kwenda kuwalinda watu wetu na virusi vya Corona,” aliyasema hayo Rais Ramaphosa akiwa amevalia sare za jeshi.
Upande wake, Banda ambaye anaendelea na program mbalimbali za mazoezi akiwa nyumbani kwake,  alichukua nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo hatari.
“Kwa huku wakikukuta unakuwa halali yao na hutakuwa na muda wa kujieleza. Natamani kuona taifa langu la Tanzania likidhibiti mapema virusi hivyo ili isifike hatua hii kwa sababu kuna watu ambao hali zao za kimaisha ni ngumu watakuwa wakila nini kwa siku  ambazo watatakiwa kukaa ndani tu bila ya kutoka nje. Mungu atusaidie,” anasema Banda.
Ligi Kuu Afrika Kusini ambako anacheza Banda ambayo ni maarufu kama PSL ilisimamishwa Machi 16 na Mwenyekiti wake, Irvin Khoza ikiwa ni jitahada za makusudi za kupunguza kasi ya maambukizi ya Corona.
Maduka ya vyakula hayatafungwa Afrika Kusini ingawa maduka ya vilevi yamepigwa marufuku wakati huu wa siku 21 za watu kubaki majumbani mwao, Waziri wa Polisi, Bheki Cel amewataka raia wa Afrika Kusini kutotumia mvinyo.