Kagere aifanya kitu mbaya Kagera Sugar, Simba yapaa kileleni

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagera akifunga bao kwa mkwaju wa penalti katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumanne ya Februari 18, 2020. Simba ilishinda bao 1-0.

Muktasari:

Ushindi huo unaifanya Simba kupaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 59, baada ya kucheza mechi 23, wakifuatiwa na Azam (44), Namungo na Yanga zinafuatiwa zikiwa na pointi 40.

Dar es Salaam. Bao la penalti ya Meddie Kagere limetosha kuipa Simba ushindi mwembamba 1-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kagere alifunga bao lake la 13, msimu huu katika dakika 60, kwa penalti baada ya nahodha John Bocco kuangushwa kwenye eneo la hatari na kipa wa Kagera Sugar, Benedict Tinocco.

Ushindi huo unaifanya Simba kupaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 59, baada ya kucheza mechi 23, wakifuatiwa na Azam (44), Namungo na Yanga zinafuatiwa zikiwa na pointi 40.

Katika mchezo huo Simba ilitawala tangu mwanzo na washambuliaji wake Kagere, Bocco wakishindwa kutumia nafasi nyingi walizopata kutokana na umakini wa kipa wa Kagera, Tinocco pamoja na safu yake ya ulinzi.

Katika kipindi cha kwanza safu ya ulinzi wa Kagera Sugar walikuwa na kazi ya ziada kupambana na washambuliaji wa Simba, Bocco na Kagere waliocheza kwa maelewano kwa kufika mara kwa mara langoni.

Nahodha wa Kagera Sugar, Juma Nyosso alicheza kwa umakini na mwenzake Erick Kyaruzi kuhakikisha nyavu zao haziguswi, lakini dakika 60 nyavu zao ziliguswa na Meddie Kagere aliyepiga penalti iliyokwenda moja kwa moja wavuni baada ya mshambuliaji mwenzake John Bocco kufanyiwa madhambi na kipa  Tinoco ndani ya boksi.

Simba iliwalazimu kutumia mbinu mbadala kuhakikisha wanapenya safu ya ulinzi ya Kagera na walianza kupiga mashuti nje ya 18.

Dakika 13, Kagere alikosa bao baada ya shuti lake kuokolewa na kipa wa Kagera Sugar, Tinocco na kuwa kona isiyokuwa na faida.

Kutokana na Simba kuonyesha kuhitaji goli la mapema kipa wa Kagera Sugar, Tinoco dakika 31 alionyeshewa kadi ya njano baada ya kuonekana kuchelewesha muda kutokana na kuomba kwenda kufunga vizuri glavu zake kwenye benchi la ufundi lakini alipofika alionyesha kuwa na mambo mengine.

Dakika 45, Simba ilikosa bao baada ya Clatous Chama kupokea pasi ya beki Shomari Kapombe huku kipa akiwa chini lakini wakati akipiga mpira huo beki wa Kagera Sugar, Erick Kyaruzi aliokoa haraka mpira huo.

Dakika 47 beki wa Kagera Sugar, Erick Kyaruzi alipewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Bocco nje ya 18 na kuwa faulo isiyokuwa na faida.

Kagera Sugar walionyesha kuhitaji goli katika kipindi cha pili baada ya kumtoa Frank Sabato dakika 52 na kuingia Awesu Awesu kwenda kuweka nguvu kwenye eneo la kiungo na Nassoro Kapama akicheza sambamba na Yusuph Mhilu katika eneo la ushambuliaji.

Mabadiliko hayo yalionyesha kuongeza nguvu kwa Kagera Sugar wachezaji wake walikuwa wanacheza kwa maelewano walikuwa wanashindwa kupenya safu ya ulinzi Simba

Dakika 59 Simba ilicheza mpira wa kushambulia kwa kushtukiza, ambapo Kagere na Luis Miquissone waligongeana pasi za haraka na kwenda kwa Bocco ambaye alikatiza katikati ya mabeki na kuingia ndani ya boksi na kufanyiwa madhambi na kipa Tinoco na mpira kuwa penalti.

Penalti hiyo ilipigwa na Kagere na kutinga moja kwa moja wavuni na kuwafanya Simba wapate goli la kuongoza huku akifikisha goli 13 msimu huu.

Kagera walifanya mabadiliko mengine dakika 68 kwa kumtoa Yusuph Mhilu na Ally Shomari huku nafasi zao zikichukuliwa na Mwaita Gereza na Peter Mwalyanzi na dakika 80 Simba walimtoa Miquissone na kuingi Hassan Dilunga na dakika 84 walimtoa Bocco na kuingia Sharaf Shiboub.

Licha ya kuwa nyuma kwa goli moja, Kagera hawakuonyesha kukata tamaa bali walikuwa wanapambana kusaka bao la kusawazisha.