VIDEO: Hii sasa sifa! Simba SC inagawa dozi kila kona Tanzania

Monday February 24 2020

Mwanaspoti, Simba SC, Yanga, Tanzania, Mwanasport, Michezo, MICHEZO, Kagere, Luis, Sven,

 

By YOHANA CHALLE

VINARA wa Ligi Kuu Bara wanatisha buana! Wakati wakiwa tayari wameshatua Shinyanga kwa ajili ya kuwahi pambano lao la Kombe la FA dhidi ya Stand United, rekodi zinaonyesha msimu huu Wekundu wa Msimbazi wako  moto kwani wanakupiga kokote unapokutana nao.
Simba ipo kileleni ikiwa imekusanya pointi 62 kutokana na mechi 24, huku rekodi zikionyesha imeshinda mara 20 na kutoka sare mbili na mbili nyingine ikipoteza na ikiweka kibindoni mabao 50 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 12 tu.
Kama Simba itaendelea na mwendo huo ni wazi huenda ikaandika rekodi ya kunyakua ubingwa wa tatu mfululizo, ikiijibu Yanga iliyofanya hivyo kuanzi 2015-2017 kabla ya kupokwa na Wekundu hao.
Hata hivyo, kama hujui ni kwamba Simba imepata pointi hizo 62 kwa kushinda kokote inapokutana na wapinzani wake, yaani nyumbani inakupiga na hata ugenini vilevile inakunyoosha.
Katika michezo 24 iliyocheza Simba imeshuka uwanja wa nyumbani mara 13 na kushinda 10, huku ikipoteza mmoja dhidi ya JKT Tanzania ngoma lililopigwa Feb 7.  Na kulazimishwa sare mbili ikiwamo ile ya 2-2 na Yanga ya Jan. 4 na suluhu dhidi ya Tanzania Prisons na kujikusanyika jumla ya alama 32.
Simba imevuna jumla ya mabao 26 kati ya 50 nyumbani na yenyewe kuruhusu nyavu zake kuguswa mara nane na katika mechi zake 11 za ugenini, rekodi zinaonyesha imeshinda 10 na kupoteza moja tu ilipocharazwa bao 1-0 na Mwadui Okt 30 mwaka jana kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Kwa maana hiyo ni kwamba Simba imevuna pointi 30 za ugenini katika mechi zake 10, huku ikifunga mabao 24 na kufungwa manne tu, kitu kinachoonyesha msimu huu Wekundu wa Msimbazi sio wa kuwachukulia poa kabisa na hasa wanapokuwa ugenini pengine kuliko nyumbani.
Hata hivyo, ieleweke mapema katika mechi nyingine za ugenini ni pamoja na zile timu zinazouitumia Uwanja wa Taifa na Uhuru vya jijini Dar es Salaam ambao Simba imevizoea viwanja hivyo na pia ndiko yalipo makao makuu yake.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sven Vanderbroek ameweka bayana kiu yake ni kutaka kuona ananyakua ubingwa na kuwa rekodi yake tangu aanze kufundisha timu ya Ligi Kuu.
“Tunatakiwa tushinde kila mchezo uliopo mbele yetu, hilo ni lengo ambalo nilianza nalo na ninataka kuendelea nalo mpaka tunachukua ubingwa msimu huu,” alisema Sven na kuelekezea mechi ya kesho ya Kombe la FA dhidi ya Stand United akidai anadhani haitakuwa rahisi kwao.
“Tunaanza na Stand United ili kuisaka robo fainali ya Kombe la FA, ila tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri, japo nadhani itakuwa mechi ngumu kwani tunacheza ugenini, kisha baada ya hapo tutarejea kwenye ligi kuikabili KMC,” alisema Sven.
Sven alisema mara baada ya mechi ya kesho Jumanne ataelekeza nguvu zake kwa mchezo wao ujao wa Ligi Kuu dhidi ya KMC utakaopigwa Machi Mosi, kabla ya kujiandaa dhidi ya Azam FC kisha Yanga Machi 8, na kote amedhamiri kupata ushindi ili kutetea ubingwa wao wa miaka miwili mfululizo.

Advertisement