Maria Sharapova atangaza kustaafu kucheza tenisi

Muktasari:

Nyota huyo wa Russia alitwaa kwa mara ya kwanza Grand Slam katika mashindano ya Wimbledon mwaka 2004 akiwa na miaka 17 alikamilisha rekodi yake ya kutwaa mataji aliposhinda French Open mwaka 2012.

London, England. Bingwa mara tano wa Grand Slam, Maria Sharapova ametangaza kustaafu kucheza tenisi akiwa na miaka 32.

Katika taarifa iliyoandika katika jarida la Vogue and Vanity Fair, Sharapova alisema mwili wake umechoka baada ya kusumbuliwa na majeruhi ya bega kwa muda mrefu.

Nyota huyo wa Russia alitwaa kwa mara ya kwanza Grand Slam katika mashindano ya Wimbledon mwaka 2004 akiwa na miaka 17 alikamilisha rekodi yake ya kutwaa mataji aliposhinda French Open mwaka 2012.

Mwaka 2016, alifungiwa miezi 15 baada ya kubainika kutumia dawa zilizokatazwa michezoni.

Tangu alipomaliza adhabu yake 2017, Sharapova ameshindwa kurudi katika ubora wake huku mara kadhaa akiwa anasumbuliwa na majeruhi.

Sharapova ameporoka hadi nafasi 373, katika viwango vya dunia, ikiwa ni kiwango chake cha chini zaidi tangu Agosti 2002, pia akipoteza mara tatu katika hatua ya awali katika mashindano matatu ya Grand Slam.