Promota adai Tyson Fury atamchapa Wilder ili azichape na Joshua

Thursday February 13 2020

Mwanaspoti, Promota adai, Tyson Fury atamchapa, Wilder azichape na Joshua

 

LONDON, ENGLAND. PROMOTA wa mchezo wa masumbwi, Frank Warren amesema Tyson Fury akimaliza tu kumtwanga Deontay Wilder atahamishia akili yake kwenye kumchapa Anthony Joshua.
Kwa mujibu wa promota Warren ni kwamba bondia Fury amepanga kutawala masumbwi ya uzito wa juu kwa mwaka huu wa 2020.
Fury na Wilder watapanda ulingoni baadaye mwezi huu huko Las Vegas, wakiwania mkanda wa WBC baada ya pambano lao la kwanza lililopigwa Desemba 2018 kumalizika kwa sare ya utata.
“Hili ni pambano kubwa zaidi ya uzito wa juu,” alisema Warren, ambaye anaamini bondia wake, Fury atamaliza rekodi ya Wilder ya kutopigwa.
“Pambano lile lililopita lilikuwa moto. Pambano hili naamini litakwenda kuwa bora zaidi. Ni suala la kuwa fiti tu kiakili na Tyson yupo fiti kwenye idara hiyo na atafanya kazi yake ya kupiga ngumi.
Pambano hilo litakapokwisha, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwaona wakipigana kwa mara ya tatu baada ya kuwapo kwa kipengele kwenye mkataba wao unasema kurudiwa kwa pamoja hilo.
Lakini, promoja Warren anaamini Fury atakuwa na pambano dhidi ya Joshua mwishoni mwa mwaka.
Joshua alirudisha ubingwa wa mikanda yake ya WBA, IBF, WBO na IBO baada ya kumtwanga Andy Ruiz Jr, Desemba, baada ya kuduwazwa kwenye pambano la kwanza alilopigana na bondia huyo wakati wa majira ya kiangazi mwaka jana.
“Atakayechapwa kwenye pambano la Fury na Wilder atakuwa na haki ya kuomba kurudiana hadi kufikia Juni,” alisema Warren.
“Ninaamini bondia wetu atashinda, hivyo itakuwa juu ya Wilder kuomba mechi ya marudiano na kinyume chake ikitokea upande huu. Wazo la maana ni kama tutaona mshindi anakipiga na AJ. Kwenye hilo, naamini Tyson atawaonyesha kuwa yeye ni bora.
Bondia Joshua ana mapambano mawili ya lazima, kwanza kuzipiga na Kubrat Pulev na kisha Oleksandr Usyk.

Advertisement