Niyonzima aipasua kichwa Gwambina mapema

Muktasari:

Mchezaji hatari zaidi Haruna Niyonzima anajua kuichezesha timu kwa utulivu pia wanaona kama atawasumbua na atachungwa ili asiwaletee madhara

LICHA ya beki wa Yanga, Juma Abdul na Ditram Nchimbi, hawazungumzwi sana mbele ya mashabiki wao, imekuwa tofauti kwa Gwambina FC, kuwaona ni hatari wakuwachunga wakikutana mechi ya Kombe la FA, itakaopigwa Jumatano ijayo.
Gwambina FC ilipiga kambi mkoani Morogoro, kujiandaa na mchezo huo, huku ikiwa na hesabu kali ya kushinda ingawa inatambua Yanga sio wepesi.
Nahodha wa timu hiyo, Jacob Massawe alisema walipata muda wa kukisoma kikosi cha Yanga na kubaini mashambulizi yake yanaanzia upande wanaokaa Abdul na Nchimbi, aliowaelezea ndio chanzo cha mabao yao ya hivi karibuni.
Alimwelezea Abdul ni fundi wa kupandisha mashambulizi yanayomkuta Nchimbi anayelazimisha akitumia nguvu kufika ndani ya 18 kwa wapinzani wake.
“Baadhi ya mechi tulizoziangalia ukiachana na walivyotoka sare mfululizo, mashambulizi yalianzia kwa Abdul na Nchimbi, ndio maana tunaona ni wachezaji wa kuwachunga zaidi,” alisema.
Mchezaji mwingine ambaye ni hatari zaidi alimtaja Haruna Niyonzima anajua kuichezesha timu kwa utulivu pia wanaona kama atawasumbua na atachungwa ili asiwaletee madhara.
“Ogopa sana kwenye timu kukiwepo mchezaji ambaye ndiye anaiendesha timu, nimeona mechi ambazo Niyonzima hajacheza Yanga imekuwa ikiyumba eneo la kiungo,” alisema.
Niyonzima alipoulizwa nini siri ya kiwango chake kinachotazamwa kama mwiba kwa wapinzani wao? Alijibu anaijua vyema ligi ya Tanzania inahitaji vitu gani.
“Asilimia kubwa ya wachezaji ambao nakutana nao kwenye ligi ni wale wale, ndio maana sioni kazi ngumu kupambana kuisaidia klabu yangu kuona tunafanya kitu cha tofauti,” alisema.