Neymar alimwa kadi nyekundu, PSG yaichapa Bordeaux

Muktasari:

Ushindi huo wa PSG dhidi Bordeaux, umewafanya kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Ufaransa kwa tofauti ya pointi 13 baada ya Marseille kukumbana na kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Nantes.

Mshambuliaji Neymar alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu Ufaransa wakati klabu yake ya Paris St-Germain ikitoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Bordeaux.

Vinara hao wa Ligue 1 walitoka sare wiki iliyopita ya mabao 4-4 dhidi ya Amiens huku wimbi la matokeo mabaya likiendelea hadi katika Ligi ya Mabingwa ambapo walikumbana na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Dortmund.

Katika mchezo huo PSG ilikuwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Parc des Princes, walianza kutanguliwa dakika ya 18 na Bordeaux walipata bao lao la kwanza kupitia kwa Hwang Ui-jo.

PSG ilibidi watumia nguvu ya ziada na hatimaye wakapata mabao mawili kabla ya kwenda mapumziko ambayo yalifungwa na Edinson Cavan na Marquinhos, Bordeaux hawakuwa nyuma nao wakakomboa kupitia kwa Pablo na kwenda mapumziko matokeo yakiwa sare ya mabao 2-2.

Matajiri hao wa Paris walienda mapumziko huku wachezaji wao wawili ambao ni Neymar na Cavan wakiwa wameonyeshwa kadi za njano.

Mambo hayakuwa magumu kwa PSG katika kipindi cha pili kwani walijipatia mabao mawili ya haraka katika dakika ya 63 na 69, yaliyofungwa na Marquinho na Kylian Mbappe, Bordeaux walipata bao lao la tatu dakika ya 83, lililofungwa na Pardo Ruben.

Kabla ya kumalizika kwa mchezo huo katika dakika za nyongeza, Neymar alijikuta akionyeshwa kadi nyingine ya njano iliyoambana na nyekundu baada ya kumchezea vibaya Yacine Adli.

Ushindi huo wa PSG dhidi Bordeaux, umewafanya kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Ufaransa kwa tofauti ya pointi 13 baada ya Marseille kukumbana na kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Nantes.