Mzamiru, Nyoni wala sio tatizo la Simba SC

Muktasari:

Simba iliondoka jana Jumapili kwenda Morogoro kucheza na Mtibwa katika mechi ya marudiano, huku zote zikiwa zimejeruhiwa, wenyeji wakitoka kupoteza mechi tatu ikiwamo ya juzi dhidi ya Lipuli, ilihali Simba ikinyooshwa na mafaande wa JKT Tanzania Ijumaa.

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck akiwa kwenye presha kutokana kuwekwa kitimoto kwa timu kushindwa kucheza vizuri na wikiendi tena kupigwa 1-0 na JKT Tanzania, kocha huyo ameanika siri ya kupoteza mchezo huo wa Ligi Kuu Bara.
Kocha Sven alisema wapinzani wao waliwazidi baada ya kukosekana kwa muunganiko wa mabeki na kiungo, lakini akisema hiyo haitokani kwa vile labda Mzamiru Yassin ama Erasto Nyoni hawapo kikosini sio tatizo la kuimfanya apate kisingizio, isipokuwa tu timu nzima inasumbuliwa na majeruhi.
Kocha huyo kutoka Ubelgiji alisema kwa sasa kikosi chake kinapitia changamoto kubwa ya kuwakosa nyota wake, lakini hawezi kutaa mchezaji mmoja mmoja kwamba kukosekana kwake ndio tatizo la kupoteza, ila ni kwamba timu imekosa muunganiko wa eneo la nyuma na katakati.
“Hata katika mchezo wa JKT tulijaribu kufanya mabadiliko eneo la kiungo na kutengeneza nafasi nyingi, ila nimeona sura tofauti za mashabiki, lakini timu ina tatizo la majeruhi,” alisema Sven.
Alipoulizwa kama kuwakosa kwake kina Nyoni na Mzamiru ni ishu kubwa, alisema anawakosa wachezaji wengi walio na matatizo kama Miraj Athuman, Shomari Kapombe, Rashid Juma na kina Erasto ambao walikuwa wagonjwa na majeruhi.
“Mzamiru aliumia tangu Januari atarudi wiki chache zijazo, Miraj aliumia akiwa na Taifa Stars akajaribu kurejea lakini hajawa fiti na anaweza akawa nje tena kwa wiki kama nne au na zaidi, huku kwa Erasto atarejea siku 10 zijazo, Kapombe na Rashid Juma wao wanaumwa,” alisema.
“Kila timu inakuwa na majeruhi na watu wanaoumwa, hivyo kukosekana kwa wachezaji hawa haimaanishi iwe kisingizo kwetu, kila mchezaji anatakiwa awe tayari kucheza muda wote ule, ndio maana ya timu na tunaenda kujipanga kwa mechi yetu ya Jumanne mjini Morogoro,” alisema.
Kuhusu kuanza kwa mawinga wake wapya Luis Misquissone na Shiza Kichuya, alisema amekoshwa zaidi na kiwango cha Luis, akiamini muda mchache atageuka kuwa mchezaji muhimu kikosini. “Ni mapema mno kuzungumzia hili kwa sababu ndio mchezo wa kwanza, ila Luis alicheza vizuri zaidi ya Kichuya na hilo lilionekana, licha ya wote kuonyesha uwezo mkubwa mazoezini.”
Simba iliondoka jana Jumapili kwenda Morogoro kucheza na Mtibwa katika mechi ya marudiano, huku zote zikiwa zimejeruhiwa, wenyeji wakitoka kupoteza mechi tatu ikiwamo ya juzi dhidi ya Lipuli, ilihali Simba ikinyooshwa na mafaande wa JKT Tanzania Ijumaa.