Molinga aanza kuisaka ahadi mabao ya Zahera Yanga

Muktasari:

Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera kwamba kama Molinga hatafunga mabao kuanzia 15 alikuwa radhi akatwe mkono ama kuwapa waliopinga Dola 1000 (zaidi ya Sh1 milioni)

Dar es Salaam. WAKATI mwenyewe akianza kuchonga kutokana na kuonekana gari lake limewaka kwenye ufungaji mabao, straika wa Yanga David Molinga amegeuka kuwa gumzo kwa wadau wa soka na wengine kuchambua uwezo wake, wakimtaja kuwa na sura mbili matata na ndiye anawabeba Jangwani kwa sasa.
Molinga aliyefunga bao pekee lililoipa Yanga ushindi na kisasi mbele ya Ruvu Shooting, alikumbushia ile nadhiri aliyoiweka Kocha wao wa zamani, Mwinyi Zahera kwamba kama hatafunga mabao kuanzia 15 alikuwa radhi akatwe mkono ama kuwapa waliopinga Dola 1000 (zaidi ya Sh1 milioni).
Akizungumza na Mwanaspoti juu ya idadi ya mabao aliyotabiriwa na Zahera, Molinga alisema isingekuwa rahisi kocha huyo kutoa kauli hiyo kama hakujua uwezo wake wa kufunga na kwamba, anataka mashabiki wasubiri waone hadi mwisho wa msimu atafunga mangapi. “Naomba baada ya msimu kumalizika niulizwe hili swali nimemaliza nikiwa na mabao mangapi, kwani naamini kama nitaendelea kupata nafasi ya kucheza nitazidi kufunga idadi kubwa kwa vile hiyo ndio kazi yangu. Kuna baadhi ya mechi za ligi mwanzo wa msimu sijacheza lakini hata hapa katikati nilipata matatizo ndani ya timu nikashindwa kuitumikia, huenda ingekuwa mbali zaidi,” alisema.
Molinga alisema kwa nafasi yake, kufunga ni jukumu lake na muhimu kwake ni kupewa nafasi na kuaminiwa kwani anadai hata alipotua Jangwani kuna waliombeza na pengine ndio maana Zahera aliwahakikisha kwamba ni mshambuliaji mzuri na mfungaji mabao mahiri.
Kwa sasa Molinga amefunga mabao saba, yakiwemo matatu aliyofunga hivi karibuni akiwa chini ya Eymael aliyemrejesha kikosini baada ya jina lake kuwekwa kwenye orodha ya waliotakiwa kutemwa.

ALIVYOCHAMBULIWA
Straika wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyezichezea Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema licha ya kuwa mfungaji bora kwa sasa wa Yanga, lakini Molinga amewagawa mashabiki na kubainika uimara na udhaifu wake kikosini.
Mogella alisema bado Molinga yupo fifte fifte kutokana na matarajio waliyoaminisha Yanga baada ya kuondoka Heritier Makambo naye kuletwa kama mbadala. “Sio mshambuliaji mbaya, ana uzuri wake ndio maana anaongoza kwa mabao kikosini, ila pia ana udhaifu wake, si aina ya mchezaji wa kuamua matokeo, hasa timu ikiwa nyuma,” alisema Mogella na kuongeza, Molinga ni mshambuliaji anayejua kwenda na muvu ya mpira ndio maana anafunga kwani hukaa sehemu sahihi mpira unapotua pale unapopigwa na wenzake.
“Mimi, nilipewa jina la Golden Boy kwa vile nilikuwa na uwezo huo na nimewahi kubadilisha matokeo katika moja ya mechi za Simba mashabiki wakiwa tayari wameanza kuondoka uwanjani wakiamini tumefungwa nikasawazisha, Molinga sio mchezaji wa aina hiyo.”
Nahodha na kiungo nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema tofauti ya Molinga ni kwamba hawezi kujitoa kama mshambuliaji kutafuta bao hasa timu ikiwa nyuma. “Ni kweli anafunga, lakini uwezo wake na kile ambacho mashabiki walikitarajia ni vitu viwili tofauti, atakuwa amemfikia Makambo kwa asilimia 60, ndio sababu bado anawapa mashaka mashabiki pamoja na kwamba anafunga,” alisema. Beki wa zamani wa Yanga, Fred Minziro alisema mshambuliaji mzuri  anaonekana kwa tabia zake uwanjani hata kama hafungi, lakini ukimuona tu anavyocheza unajua ni hatari.