Mkwasa ashtukia kuna mkono wa Simba Tanga, Yanga ikivaa Coastal Union

Muktasari:

Kocha Mkwassa amesisitiza wanaipa umuhimu mkubwa mechi hiyo na wanaamini leo ndio mwanzo wa kurudi kwenye rekodi zao za ushindi

TANGA. KOCHA Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa amesema wanaelewa kila kitu Simba wanachoombea kwenye mechi yao na Coastal Union leo Jumapili, jijini hapa.
Mkwasa ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga, ameweka wazi wanajua si tu Simba watajazana Mkwakwani leo kuwaombea mabaya, bali hata mitaani wanatamani wafungwe au wakose pointi kabisa, lakini wao watakaza kwelikweli.
Yanga imetoa sare tatu mfululizo katika mechi za mwisho za ligi. Kocha huyo amesisitiza wanaipa umuhimu mkubwa mechi hiyo na wanaamini leo ndio mwanzo wa kurudi kwenye rekodi zao za ushindi kwa vile kila mmoja amepania kufuta wimbi la sare.
Mkwasa aliliambia Mwanaspoti mazoezini kwenye Uwanja wa Popatlal; “Tunafahamu joto lililopo kuhusu mechi hii hapa Mkwakwani na tunajua fika wapinzani wetu wa jadi wanavyoomba dua ili tufungwe, lakini hapa tunataka na alama zetu tatu na tumejipanga vizuri kufanya hivyo. Hatuna wasiwasi.”
Mkwasa ambaye miaka ya nyuma aliwahi kuifundisha Coastal Union alisema anaifahamu vyema timu hiyo na atatumia uzoefu wake kupata ushindi na kuziba kelele za Simba inayoongoza msimamo wa ligi ikitaka kutwaa ubingwa mapema na kwa pointi nyingi.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesisitiza kila kitu kwa upande wao kipo sawa na amewahakikishia mashabiki uhakika wa ushindi upo na kuanzia leo wanarudi kwenye kasi yao.
“Sare siyo kitu kizuri kwa mashabiki, lakini tunawaomba waje kuiunga mkono timu yao, sisi tumeshazungumza na wachezaji na benchi la ufundi kila kitu kiko sawa,” alisisitiza kiongozi huyo wa zamani wa TFF na Mtibwa Sugar.
Juma Mgunda ambaye ni Kocha wa Coastal Union alisema baada ya wachezaji wake kumaliza mazoezi katika uwanja wa Mkwakwani; “Yanga tunaiheshimu ni timu kubwa nchini na kongwe katika ligi hii lakini tutahakikisha tunaifunga.”
Mwanaspoti ilishuhudia katika viwanja vyote mashabiki wakiwa wengi huku wakitambiana kila upande kuwa utatoka na ushindi ambapo Yanga wameonekana kwa wingi mitaani na magari yao kutoka Dar es Salaam na mikoa ya jirani.