Mbao yampa zawadi Ndayiragije kwa kuichapa Singida United

Muktasari:

Ushindi huo umeifanya Mbao kufikisha pointi 25, huku Singida United wakibaki na alama zao 11 na kuendelea kuburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Mwanza.Jahazi la Singida United linazidi kuzama baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Mbao FC huku kocha wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije akishuhudia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mbao FC ikicheza bila makocha wake, Hemed Morocco na Msaidizi wake, Abdulmutiki Khaji waliotangaza kung'atuka kutokana na hali ngumu ya maisha kwa wachezaji ilitumia vizuri uwanja wake dhidi ya vibonde wenzao Singida United.

Ushindi huo umeifanya Mbao kufikisha pointi 25, huku Singida United wakibaki na alama zao 11 na kuendelea kuburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Mbao ilipata bao la kwanza katika dakika ya 21 kupitia kwa Mussa Haji akitumia vyema pasi ya Helbert Lukindo kabla ya Lukindo kufunga bao la pili dakika ya 39 akiunganisha mpira wa Waziri Junior na kuwachanganya kabisa wapinzani.

Singida United ilikumbana na pigo hicho wakiwa pungufu baada ya mchezaji wao, Elinyesya Sumbi kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya beki wa Mbao, Iganas Juma.

Mbao FC ilitumia pengo hilo kupata bao la tatu katika dakika ya 66, kupitia Jordan John kabla ya Daud Mbweni kuifungia Singida United bao la kufutia machozi katika dakika za nyongeza.

Ushindi huo wa Mbao ni kama ulikuwa maalumu kwa aliyewahi kuwa Kocha wao Mkuu, Ndayiragije ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha timu ya Taifa 'TaifaStars' aliyeshuhudia mechi hiyo kwa dakika 90.