Lamine, Niyonzima, Molinga kuikosa Namungo, GSM, Yanga kimeeleweka

Muktasari:

Yanga wenye pointi 50, wapo nyuma ya Azam (54), Namungo ipo nafasi ya nne wakiwa na pointi 49 kabla ya mchezo huo wa leo.

Dar es Salaam. Beki Lamine Moro na kiungo Haruna Niyonzima ni miongoni mwa nyota wa Yanga watakaokosa mechi ya leo Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema sababu ya wachezaji hao walishindwa kusafiri na timu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo majeruhi.

"Niyonzima alishindwa kusafiri na timu kwa sababu anatumikia kadi tatu za njano hivyo hata kama angesafiri asingetumika katika mchezo huo, Lamine na Molinga ni wagonjwa," alisema Ofisa hiyo.

Kocha wa timu hiyo, Luc Eymael baada ya kumaliza mazoezi hapo jana, aliwatolea uvivu baadhi ya wachezaji wake mbele ya vyombo vya habari mkoani Lindi kwa kusema wanakosa sifa ya kuwa wachezaji wa kulipwa.

“Kuna wachezaji ambao sikubaliani nao kwa kushindwa kwao kusafiri na timu, wapo ambao nina taarifa zao kwa  mfano Adeyum na Banka na wengine wanaotumikia adhabu (Niyonzima) na  kusumbuliwa na majeraha (Lamine na Molinga), wengine wanachagua mechi, hiyo sio heshima," alisema.

Molinga ambaye ni raia wa DR Congo hatacheza mechi ngumu ya leo dhidi ya Namungo mkoani Mtwara na hakuwepo kabisa kambini tangu mechi na KMC imalizike kwenye Uwanja wa Uhuru.

Kitendo hicho pamoja na matukio yake ya hivi karibuni vimemkera Kocha Luc Eymael na viongozi.

Molinga anakabiliwa na tuhuma za utovu wa nidhamu na awali alianza kumtibua kocha wakati timu hiyo ikisafiri kuwafuata Polisi Tanzania akidai anaumwa kabla ya benchi kujiridhisha alikuwa anazuga tu.

Baada ya hapo alikosa mechi takribani nne ile ya Polisi, Coastal Union zote za ugenini kisha hata aliporejea mazoezini katika maandalizi dhidi ya kuivaa Mbao na baadaye Simba, benchi hilo lilimfungia vioo wakimweka jukwaani kama shabiki.

Mshambuliaji huyo aliyeifungia Yanga mabao manane msimu huu akiwa ndio mfungaji mwenye mabao mengi kikosini, alilitibua tena Machi 12 walipomaliza mchezo dhidi ya KMC na baada ya kutocheza vizuri kisha kusakamwa na mashabiki alikacha kurejea kambini.

Hatua hiyo imewatibua sio tu makocha bali hata mabosi wa timu hiyo na Mwanaspoti limejiridhisha Eymael ameshawaambia mabosi wa klabu hiyo jamaa atakuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kumwonyesha mlango wa kutokea msimu ukimalizika.

GSM Fresh Yanga

Yanga imeithibitishia imefikia hatua nzuri kwenye ishu ya GSM kuongeza mkataba wenye ulaji mnono zaidi Jangwani.

Awali Yanga iliingia mkataba wa miaka miwili na GSM ule wa kuwauzia jezi zao ambazo zinasumbua sokoni kwa sasa pamoja na udhamini mwingine wa matangazo ya magodoro yao.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alifafanua kwa kifupi; “Tunaridhika na jinsi tulivyoshirikiana na GSM, wamekuwa ni watu muhimu kwetu katika kipindi kifupi tulichokuwa nao, pia kuhusu kuongeza mkataba wa udhamini ni kweli kuna taratibu zimeanza kuwaongezea muda zaidi.”

Habari za ndani zinasema Yanga wameamua kuongeza dili la GSM ambaye amekubali kushiriki kwenye mchakato wa kuibadili klabu hiyo kuwa ya kisasa zaidi pamoja na kusuka kikosi kipya cha msimu ujao.

Habari zinasema kampuni hiyo itaweka dau nono ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa shughuli za uendeshaji wa timu wakishirikiana na wadhamini wengine.