Kocha Eymael aanza kuiondoa Yanga katika mbio za ubingwa Ligi Kuu Tanzania

Sunday February 23 2020

Mwanaspoti, Kocha Eymael, Yanga, Mwanasport, Simba, ubingwa, Ligi Kuu, Tanzania

 

By THOMAS NG’ITU

KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael ameanza kupiga hesabu mpya za kutaka nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu Bara huku akifananisha mchuano wa msimu huu na ule wa Ligi Kuu ya England.
Luc ameliambia Mwanaspoti kwa namna ambavyo ligi inakwenda ni vigumu moja kwa moja kusema utachukua ubingwa.
“Ligi ni ngumu kiukweli hata kama unaitaka nafasi ya kwanza, binafsi nafikiria nafasi zote tatu za juu lakini kuna changamoto pia ya kumshusha Azam anayeshika nafasi ya pili,” alisema kocha huyo mwenye uzoefu na soka la Afrika.
Luc alisema ugumu wa ligi ya Tanzania na namna ambavyo timu zimetofautiana pointi ni kama Ligi Kuu ya England.
“Ukiangalia Liverpool wana pointi nyingi sana, wanafuata Man City na Leicester City nadhani sasa ukija kuangalia na huku ni hivyohivyo lakini bado kotekote timu zinapambana mpaka mwisho,” alisema.
“Mechi tunacheza  mfululizo sana, kwahiyo lazima uwe unafanya mabadiliko katika kikosi ili kuweza kuendana na ligi inavyokwenda.”
Yanga inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 40, Namungo  nafasi ya tatu pointi 43, huku Azam FC wakiwa na pointi 45 wakiwa nafasi ya pili na nafasi ya kwanza ikishikwa na Simba wakiwa na pointi 62.

Advertisement