Kenya ni kicheko Olimpiki kuahirishwa Japan 2020

Muktasari:

Siku ya Jumanne, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Thomas Bach na Waziri Mkuu wa Japan, Abe Shinzo, walifanya mkutano na waandishi wa habari na kuitangazia dunia kuwa, michezo hiyo sasa itafanyika mwakani, sababu ikiwa ni tahadhari ya Covid-19.

KENYA. Kamati ya taifa ya Olimpiki (NOC-K), Shirikisho la Riadha (AK) na ile ya mchezo wa Voliboli (KVF), ni kati ya mashirikisho yaliyopokea kwa shangwe taarifa za kuahirishwa kwa Michezo ya Olimpiki 2020.
Awali taifa la Japan, ambao ndio wenyeji wa makala haya, pamoja na kamati ya kimataifa ya Olimpiki (IOC), walikazia kuwa michezo hiyo, itaendelea kama ilivyopangwa licha ya hofu ya ugonjwa wa Corona, ambayo imeshasababisha vifo vya maelfu ya watu duniani kote.
Hata hivyo, siku ya Jumanne, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Thomas Bach na Waziri Mkuu wa Japan, Abe Shinzo, walifanya mkutano na waandishi wa habari na kuitangazia dunia kuwa, michezo hiyo sasa itafanyika mwakani, sababu ikiwa ni tahadhari ya Covid-19.
“Tumefurahi sana kupokea taarifa hizi. Hii ni habari nzuri kwa wanariadha wetu, tulikuwa tunahofia usalama wao, maana hali kwa kweli ni mbaya sana na ilivyo ni ngumu kwa ugonjwa huu kudhibitiwa kabla ya Julai,” alisema Rais wa NOC-K, Paul Tergat.
Tergat, ambaye alikiri kuwa, awali alikuwa amefanya mawasiliano na Bach, kuhusu suala hilo, alisema kuwa kusitishwa kwa shughuli za michezo na mkusanyiko wa watu, pamoja na agizo la watu kukaa majumbani, kuliwafanya wanariadha kusitisha mazoezi.
Katibu Mkuu wa NOC-K, Francis Mutuku alidokeza kuwa, kati ya wanariadha 11,000 wanaotarajiwa kuwakilisha Kenya Jijini Tokyo, ni asilimia 47 tu ndio waliofuzu michezo hiyo kwa hiyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
Rais wa Voliboli, Waithaka Kioni, alisema KVF imefurahishwa na uamuzi huo wa IOC.