Aston Villa ya Samatta yakubali kipigo cha Spurs

Muktasari:

Katika mchezo huo kocha wa Spurs, Jose Mourinho alimpangia Samatta mabeki wa kati wawili wakorofi Toby Alderweireld na Davinson Sanchez,

London, England. Mshambuliaji Mbwana Samatta amecheza kwa dakika 83 na kushindwa kuisaidia Aston Villa kuepuka kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Tottenham Hotspur kwenye Uwanja wa Villa Park.

Katika mchezo huo kocha wa Spurs, Jose Mourinho alimpangia Samatta mabeki wa kati wawili wakorofi Toby Alderweireld na Davinson Sanchez, lakini bado straika huyo Mtanzania alifanya makeke na kusababisha beki wa Alderweireld kujifunga katika dakika ya tisa kuwafanya Aston Villa kupata bao la kuongoza.

Hata hivyo, Alderweireld baadaye alienda kurekebisha makosa yake ya kufunga bao la kusawazisha kwenye dakika ya 27.

Lakini, staa wa Korea Kusini, Son Heung-min, ndiye aliyeamua matokeo ya mchezo huo baada ya kufunga mara mbili, likiwamo bao ya dakika za majeruhi lililowafanya Spurs kukusanya pointi tatu zinazowafanya wabakize moja tu kutinga Top Four.

Bao jingine la Aston Villa, ambalo lilikuwa la kusawazisha lilifunga na Bjorn Engels.

Kwa matokeo hayo, Samatta, hakumaliza mechi hiyo anaendelea kusubiri ushindi wake wa kwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu England akiwa na kikosi chake cha Aston Villa, kinachoshika nafasi ya 18 kwenye msimamo, pointi moja tu juu ya timu zilizopo kwenye hatari ya kushuka daraja. Sambamba na hilo, Samatta ameshindwa kumnyamazisha kocha mwenye rekodi zake duniani, Mourinho.

Vikosi

Aston Villa XI: Reina, Engels, Konsa, Hause, Guilbert, Drinkwater, Douglas Luiz, Targett, El Ghazi, Samatta, Grealish

Aston Villa akiba: Borja Baston, Taylor, Nakamba, Hourihane, Trezeguet, Nyland, Elmohamady

Tottenham Hotspur XI: Lloris, Aurier, Sanchez, Alderweireld, Davies, Winks, Dier, Lucas Moura, Alli, Bergwijn, Son

Tottenham akiba: Vertonghen, Lo Celso, Gazzaniga, Ndombele, Skipp, Fernandes, Tanganga.

Mwamuzi: Martin Atkinson (W Yorkshire)