Mwanafunzi Omalla mchezaji bora wa Ligi Kuu Kenya Desemba

Wednesday January 29 2020

 

By Fadhili Athumani

Kisumu, Kenya. Straika wa Western Stima, Benson Ochieng Omalla mwenye umri wa miaka 17, ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu Kenya (KPL), kwa mwezi wa Desemba.

Omalla ni mwanafunzi wa shule ya upili ya Kisumu Day High, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi, kushinda tuzo hiyo inayotolewa na chama cha Waandishi wa habari wa michezo nchini (SJAK).

Katika umri wake mdogo wa miaka 17, mwanafunzi huyo wa kidato cha nne, ametwaa tuzo hiyo inayotolewa kila mwezi kutambua mchango wa wachezaji, baada ya kufunga jumla ya mabao sita mwezi wa Desemba.

Tofauti na ilivyo desturi ambapo SJAK hukabidhi tuzo, wakati wa mazoezi ya timu, Omalla, ambaye mpaka sasa yuko kwenye rada ya Jedwali la mfungaji bora wa KPL, akiwa na mabao saba, alikabidhiwa tuzo yake, wakati wa mapumziko (breaktime), mbele ya wanafunzi wenzake.

Kwa kuibuka mchezaji bora wa mwezi Desemba, Omalla alikabidhiwa kombe na zawadi ya runinga ya kisasa yenye ukubwa wa 49inch, kutoka kampuni ya LG katika mwezi wa Desemba, Omalla alifunga bao lake la kwanza la msimu dhidi ya KCB.

Mabao yake mengine, aliyafunga dhidi ya Zoo Kericho, ambayo aliitungua mara tatu (hat-trick), kabla ya kuifungia Western Stima mabao mawili dhidi ya Nzoia Sugar. Western Stima hivi sasa inashika nafasi ya saba kwenye jedwali ikiwa na pointi 30.

Advertisement

Advertisement