Mwamuzi Simba, Al Ahly huyu hapa mwanangu

Muktasari:

  • Simba wanatarajia kushuka uwanja wakiwa na kumbukumbu ya kukubali kipigo cha bao 5-0 dhidi ya Al Ahly ugenini na wao watakuwa wenyeji katika mchezo huo ukiwa ni wa nne katika kundi lao.

Dar es Salaam. Mwamuzi Mahmood Ali Ismail atachezesha mechi marudiano Kundi D Ligi ya Mabigwa Afrika kati ya Simba na Al Ahly itakayochezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, saa 10 jioni.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limemteua mwamuzi huyo wa Sudan atasaidiana na Waleed Ahmed Ali na Ahmed Nagei Subahi.

Mchezo huo utafanyika siku chache baada ya Simba ikubali kichapo cha mabao 5-0 na Al Ahly Jumamosi ya Februari 2, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria, Misri.

Mchezo mwingine wa Kundi D siku hiyo kati ya JS Saoura na AS Vita Uwanja wa Agosti 20, 1955 mjini Bechar nchini Algeria utachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda, Louis Hakizimana atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Ambroise Hakizimana na Justin Karangwa.

Ikumbukwe mechi ya kwanza baina ya timu hizo ilimalizika kwa kwa sare ya 2-2 Uwanja wa Martyrs de la Penteccte mjini Kinshasa, AS Vita wakitangulia kwa mabao ya Kazadi Kasengu dakika ya 14 na Jean-Marc Makusu Mundele dakika ya 37, kabla ya JS Saoura kusawazisha kupitia kwa Mohamed El Amine Hammia kwa penalti dakika ya 45 na Sid Ali Yahia Cherif dakika ya 88.

Baada ya mechi za mzunguko wa kwanza, Al Ahly inaongoza Kundi D kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na AS Vita yenye pointi nne, Simba SC pointi tatu na JS Saoura wanashika mkia kwa pointi zao mbili.