Mwamuzi Jonesia aweka rekodi mpya Afrika

Wednesday March 13 2019

 

Dar es Salaam. Wakati fainali za Mataifa ya Afrika U-17, zikitaraji kuanza kutimua vumbi mwezi ujao, wenyeji Tanzania wameweka rekodi ya kutoa mwamuzi wa kwanza mwanamke kucheza fainali hizo.

Hii ni mara ya kwanza kwa CAF kumtangaza mwamuzi mwanamke, Jonesia Rukyaa Kabakama kuchezesha fainali za mataifa ya Afrika kwa wanaume.

Mwamuzi Jonesia ni miongoni mwa waamuzi 29, waliochaguliwa kwa ajili ya kufanya mafunzo ya kujianda kuchezesha mashindano hayo. Mafunzo hayo yatafanyika jijini Casablanca, Morocco kuanzia Machi 31 hadi Aprili 4, 2019.

Baada ya mafunzo hayo kutatangazwa orodha ya mwisho kwa ajili ya kucheza fainali hizo za wiki mbili jijini Dar es salaam.

Mwamuzi Jonesia atakuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na Njoroge (Kenya) pamoja na Rakotozafinoro (Madagascar).

Mwamuzi Jonesia atakuwa mmoja wa waamuzi 15 wa kati, pamoja na Nabi Boukhalfa (Algeria), Issa Sy (Senegal), Dahane Beida (Mauritania), Mashood Ssali (Uganda) na Mlibya Huraywidah Abdulwahid.

Wengine ni Thirelo Mositwane (Botswana), Blaise Yuven Ngwa (Cameroon), Mahrous A.H. Ahmed (Egypt), Mogos Teklu Tsegay (Eritrea), Atcho Pierre (Gabon), Andofetra Rakotokojaona (Madagascar), Samir Guezzaz (Morocco), Basheer Salisu (Nigeria), Karim Twagirumukiza (Rwanda).

Waamuzi wasaidizi ni; Thomas Kusosa, Hassan Khalil, Mohamed Mkono, Aymar Ulrich Eric Ayimavo, Habib Judicarel Sanou, Brahim Adam Ahmat, Salah Abdi Mohamed, Nouha Bangoura, Youssef Wahid Elbosaty, Mary Wanjiru Njoroge, Lidwine Rakotozafinoro, Reis Dos Montengero Miro, James Emile na Ahmed Omer Hamid.

Nchi nane zimefanikiwa kufuzu kwa fainali hizo na zimepangwa katika makundi mawili.

Tanzania ipo Kundi A pamoja na jirani zao Uganda, Nigeria, na Angola. Kundi B linaundwa na Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.

Mashindano hayo yataanza kutimua vumbi Aprili 14 na kumalizika Aprili 28, 2019.

Timu nne zinazofikia nusu fainali zinafuzu moja kwa moja kucheza Kombe la Dunia FIFA U-17, nchini Peru kuanzia Oktoba 5 hadi 27, 2019.

Timu zilizofuzu kwa fainali za Peru hadi sasa ni pamoja na Australia, Japan, Korea Kusini, Tajikistan, New Zealand na Solomon Islands.

Advertisement