Mwambusi aanika mipango yake Mbeya City

Muktasari:

Mwambusi amesema baada ya mazoezi hayo ya gym yatakayoanza Jumatatu ataingia mazoezi ya uwanjani na baada ya wiki mbili watacheza mechi za kirafiki.

KOCHA wa Mbeya City, Juma Mwambusi ameweka wazi programu yake ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kwamba ataanza na mazoezi ya utimilifu wa mwili yatakayofanyika kwa siku tatu.
Mwambusi ambaye aliipandisha timu hiyo daraja amerudi kuchukuwa nafasi ya kocha Ramadhan Nswanzurwino raia wa Burundi aliyemaliza mkataba wake.
Mwambusi amesema baada ya mazoezi hayo ya gym yatakayoanza Jumatatu ataingia mazoezi ya uwanjani na baada ya wiki mbili watacheza mechi za kirafiki.
"Nimeuomba uongozi kututafutia japo timu za nje ya mkoa kwa ajili ya mechi za kirafiki kuelekea msimu mpya, kambi yetu itakuwa hapa hapa jijini Mbeya maana kila kitu kinapatikana hapa.
"Kwa asilimia kubwa usajili wetu upo tayari, tumeanza maandalizi hasa kwa kliniki ya vijana ambao wengine tutawaongeza kwenye kikosi cha timu ya vsijana kwani kuna baadhi tunawapandisha timu ya wakubwa, lazima tuwe na timu ya vijana iliyo imara itakayotusaidia kwenye usajili hapo baadaye," anasema Mwambusi
Katika mazoezi yanayoendelea kwa vijana watakaosajiliwa ni kukimbia kilomita 3 ambayo ameeleza kwamba yatasaidia kuwaweka sawa kwenye utimamu wa mwili.