HISIA ZANGU : Mwalimu nyerere hakutuachia akili za Samatta na Diamond

Muktasari:

Wanamichezo wengi hawafahamu kwamba michezo ni ajira. Hawafahamu kwamba michezo ni kazi ya kupona. Hawafahamu kwamba vipaji walivyopewa ni zaidi ya utajiri. Ndio maana mpaka leo hawako makini na kazi zao.

JANA Mwalimu Nyerere ametimiza miaka 20 tangu aondoke. Nyakati zimekwenda wapi? Ni muda mrefu sasa. Mwalimu alikuwa mjamaa haswa. Huku katika michezo ameacha makovu mazito ya ujamaa ambayo ni magumu kufutika.

Ni huyu huyu Mwalimu aliyetuambia tupendane. Ni huyu huyu Mwalimu ambaye aligawa madaftari bure shuleni enzi hizo. Ni huyu huyu Mwalimu ambaye katika michezo aliunda timu zake za mashirika ambazo zilitamba katika michezo tofauti.

Ni huyu huyu Mwalimu ambaye chini yake wanamichezo wa majeshi walitamba sana. Ni Mwalimu huyu huyu ndiye ambaye katika utawala klabu za Simba na Yanga zilifanikiwa kujenga majengo yake. Yanga wakajenga na uwanja kabisa. Kabla hajafariki maisha yalibadilika. Tukahama kutoka katika ujamaa tukaenda katika ubepari.

Hapo ndipo katika michezo kila mtu alipigwa chenga. Hatukuweza kumudu tena kasi ya ubepari katika michezo yote. Wanamichezo wetu hawakuweza tena kumudu kasi. Katika soka hali bado ni mbaya. Walioamua kwenda sawa na kasi ya ubepari ni wachache. Akina Mbwana Samatta na Simon Msuva.

Wanamichezo wengi hawafahamu kwamba michezo ni ajira. Hawafahamu kwamba michezo ni kazi ya kupona. Hawafahamu kwamba vipaji walivyopewa ni zaidi ya utajiri. Ndio maana mpaka leo hawako makini na kazi zao.

Mchezaji anakubali kufanywa shabiki au mwanachama katika klabu yake. Mchezaji haamini kama anaweza kufanya mambo yake mwenyewe na kuishi kwa ajili ya familia yake. Bado kuna wachezaji wanaambiwa wasaini mikataba huku wakiambiwa ‘Wewe ni Yanga, wewe ni mwenzetu, saini hapa wiki ijayo tutakulipa pesa zako’. Haya yalikuwa maisha ya kijamaa waliyoishi kina Said Mwamba lakini mpaka leo wengine wanaishi.

Wachezaji wengi, hasa mastaa wana uhakika wa kutembea mitaani na kupewa pesa, kununuliwa bia, au kula. Haya ni maisha ya kijamaa ambayo mpaka leo yapo. Hata hivyo mpira wa leo unataka uwe bepari. Wachezaji wetu hawataki kupambana nje na kupata pesa nyingi kwa sababu ukiwa staa Bongo maisha yanakwenda. Unapewa pesa nyingi nje ya mkataba wako.

Katika klabu, bado hatukuandaliwa kuishi kibepari. Baada ya Mwalimu kufa na timu zake za mashirika na majeshi, hatukujua ni namna gani klabu ya soka inapaswa kuendeshwa kibepari. Klabu zikaendeshwa kwa kutegemea ufadhili na michango ya wanachama pamoja na viingilio vya mechi.

Inapokuja timu kama Al Ahly huwa tunashangaa jinsi ambavyo jezi za timu yao zimechafuka kwa matangazo. Ule ni ubepari mkubwa. Sisi hatukuandaliwa kuishi hivyo. Hatukuandaliwa kuwa na watu wa masoko ambao wanahenya kwa ajili ya kuitangaza timu.

Hii sio kwa Simba na Yanga tu. Mpaka leo timu kama Coastal Union, African Sports, Pamba, Tukuyu Stars na zile kongwe za zamani zimeshindwa kujigeuza kuwa Manchester City au PSG. Zimeshindwa kuingia katika mfumo mpya wa kibepari.

Wakati ule Coastal Union ingeweza kumsajili Juma Mgunda kwa kumpatia feni ya ukutani tu, leo mchezaji wa maana anataka Sh 40 milioni na mkataba wa miaka miwili tu. Viongozi wetu wa sasa hawakujiandaa kwa maisha haya. Walijiandaa kwa maisha yale yale ya Mwalimu. Maisha ya kumchukua mchezaji kwa maneno kwa sababu baba yake alikuwa shabiki wa Coastal zamani.

Hata huku katika muziki inaonekana ni Diamond Platnumz ndiye aliyejiandaa zaidi kuishi kibepari. Hakujali sana suala la kipaji. Hatimaye aliweza kumzawadia gari marehemu Muhidin Gurumo ambaye aliathiriwa na sera za ujamaa akajikuta anatumbuiza bure katika shughuli za chama na serikali.

Kama Mwalimu angepata nafasi, nadhani angetutahadharisha sisi wa upande wa michezo tujiandae na mfumo mpya wa maisha. Mfumo wa kibabe ambao unataka kila mwanadamu ajitegemee zaidi na familia yake. Mfumo ambao ungezitaka klabu zijiandae kwa kujitegemea zaidi.

Mfumo wake ulituletea wanamichezo wengi mahiri katika kila mchezo, lakini hakujiandaa tena kutengeneza wanamichezo wa aina hii nje ya majeshi na mashirika. Ndio maana leo tunahaha. Hatuna sehemu ya kushika. Tuliua ujamaa tukaingia katika ubepari bila ya kuandaa akili za Watanzania.

Leo ukiwaambia timu inaweza kumilikiwa na mtu mmoja watu wanatumia akili za ujamaa kukataa jambo hilo. Lakini mashirika mengi ya Mwalimu yalipekwa katika mikono ya watu binafsi kwa sababu ya ubepari. Tusingeweza kubishana na nyakati. Lakini leo bado tunabishana na nyakati kwa kutumia akili za kijamaa.

Kama Mwalimu angepewa nafasi ya kutusimulia vema kuhusu ubepari unavyofanya kazi, nadhani leo tungekuwa na kina Diamond wengi. Kina Samatta wengi. Alituacha kama tulivyo katika ujamaa na wengi tunaishi katika ujamaa ingawa mambo yamebadilika. Bado kuna mchezaji anayekataa dili la kwenda klabu kubwa ya Afrika kwa sababu ya kupenda tu kushangiliwa Uwanja wa Taifa huku akiingiza visenti vichache. Makovu ya ujamaa.