Mwalala: Mje muone mabao yanavyotupiwa

Muktasari:

Asha alibatizwa jina la Mwalala kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao akifananishwa na Benard Mwalala ambaye sasa ni kocha mkuu wa Bandari FC ya Kenya. Enzi zake, Mwalala alipiga sana mabao alipokuwa anaichezea Yanga.

MKALI wa mabao wa timu ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’, Asha Rashid ‘Mwalala’ amewataka wanaosema soka ni la wanaume wafike uwanjani waone wanavyowapiga watu mabao, na akasisitiza kikosi chao kitaweka rekodi ya kutwaa Kombe la Cecafa mara ya tatu mfululizo.

Asha alibatizwa jina la Mwalala kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao akifananishwa na Benard Mwalala ambaye sasa ni kocha mkuu wa Bandari FC ya Kenya. Enzi zake, Mwalala alipiga sana mabao alipokuwa anaichezea Yanga.

Mchezaji huyo wa Kilimanjaro alisema anapata nguvu ya kuzungumza hayo kutokana na namna walivyojipanga kuwa vizuri.

“Kila kitu kinawezekana, sipendi maneno mengi na ninachosisitiza watu wajitokeze kwa wingi kwenye mashindano haya ili washuhudie burudani ya nguvu,” alisema Asha.

Alisema wadau watapofika kwa wingi na kujionea kwa macho yao pia, watawapa nguvu ya kufanya vizuri zaidi katika mashindano hayo.

“Unaposikia watu wanakusapoti nje halafu upo nyumbani raha, waje wengi na hawatajutia,” alisema Asha.

Akizungumzia rekodi ya kutwaa ubingwa mara tatu, Asha alisema ndio malengo yao. “Ndicho tulichokikusudia Cecafa.”