Mwalala: Gor Mahia waliangukia tu buda

Muktasari:

Kwenye mchuano huo, Bandari ilionyesha mchezo mzuri sana ikimiliki mechi kwa asilimia kubwa kuliko wapinzani, ila bahati iliikwepa na kuiangukia Gor iliyofanikiwa kufunga goli la kipekee kunako dakika ya 64.

AISEE! Kocha wa Bandari FC Bernard Mwalala mbishi kinoma.

Mwalala hajakubali kushindwa licha ya timu yake kuangukia kichapo cha goli 1-0 dhidi ya Gor Mahia zilipochuana kwenye fainali ya Super Cup juzi Jumapili uwanjani Kenyatta mjini Machakos.

Mabingwa hao wa taji la ligi Kuu na Kombe la GOTV Shield Cup msimu uliopita ambao pia ni wawakilishi wa taifa kwenye mashindano ya CAF Champions League na CAF Confederation, walichuana kwenye mchuano huo wa kuukaribisha msimu mpya wa 2019/20 unaotarajiwa kuanza Jumamosi ya wiki hii.

Kwenye mchuano huo, Bandari ilionyesha mchezo mzuri sana ikimiliki mechi kwa asilimia kubwa kuliko wapinzani, ila bahati iliikwepa na kuiangukia Gor iliyofanikiwa kufunga goli la kipekee kunako dakika ya 64.

Bao hilo lilipachikwa wavuni na Lawrence Juma baada ya kuangukia mpira uliotemwa na kipa wa Bandari, Michael Wanyika baada yake kuipangua krosi yake nahodha wa Gor, Kenneth Muguna kutoka kulia mwa uwanja.

Na hata baada ya kiungo wa Gor Tobias Otieno kulishwa kadi nyekundu kunako dakika ya 77, Bandari ilijitahidi kuibana lakini wapi.

Licha ya matokeo hayo, Kocha Mwalala alibaki kuchocha tu akidai kuwa wapinzani wao waliangukia lile goli.

“Kwa kweli waliangukia tu, shoti moja na ikawapa goli. Lakini ukitizama mechi nzima kiufundi na kimbuni tuliwachezea sana mzee. Nafikiri haikuwa siku yetu sababu Gor tumezoea kuwalemea tangu zamani na daima huwezi ukatesa siku zote kwa kufululiza,” Mwalala akamimina.

Hata hivyo, kinachomfurahisha zaidi ni kupevuka kwa mchezo wa vijana wake akilinganisha na viwango walivyoonyesha walipochuana na Al Shandyy wa Sudan kwenye dimba la CAF Confederation mkondo wa kwanza wikendi iliyopita uwanjani Nyayo.

Mechi hiyo iliishia sare tasa na Kocha Mwalala alibaki kuwacharukia viungo wake kwa kuiza timu kutokana na kile alichokitaja kiwango duni.

“Siwezi kulalamikia kupoteza hasa zaidi baada ya kuona kiwango chetu kilivyoboreka nikilinganisha na mchuano dhidi ya Al Shandy. Hakika tulicheza vizuri sana dhidi ya Gor kinyume na ilivyokuwa na Al Shandy. Tunapostahili kukaza buti sasa ni kwenye safu ya mashambulizi,” Mwalala akaongeza.