Mwalala: Bandari itachapa Wazito FC

Muktasari:

Mkufunzi huyo ambaye ana hamu kubwa ya timu yake kupata ushindi baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa mechi nane zilizopita, aliambia Mwanaspoti kuwa ingawa aliwakosa wachezaji wake sita wa kikosi cha timu ya kwanza, wale waliocheza walimridhisha na ana imani watacheza vizuri zaidi kesho.

MOMBASA. BANDARI FC imeeleza ina matumaini asilimia kubwa ya kupata ushindi kwenye mechi yao ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) dhidi ya Wazito FC itakayopepetwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Mbaraki Sports Club hapo kesho Ijumaa.

Kocha Mkuu wa Bandari FC, Bernard Mwalala amesema ana matumaini makubwa wachezaji wake kujituma zaidi ya walivyofanya walipokutana na Tusker FC na kushindwa kwa bao 1-0 uwanja wa Ruaraka jijini Nairobi mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Nina imani kubwa kama tuna uwezo wa kupata ushindi dhidi ya wageni wetu Wazito kwani mchezo tuliocheza dhidi ya Tusker uliniridhisha na sasa natarajia pakubwa kwa timu kupata ushindi katika mechi yetu ya Ijumaa,” akasema Mwalala.

Mkufunzi huyo ambaye ana hamu kubwa ya timu yake kupata ushindi baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa mechi nane zilizopita, aliambia Mwanaspoti kuwa ingawa aliwakosa wachezaji wake sita wa kikosi cha timu ya kwanza, wale waliocheza walimridhisha na ana imani watacheza vizuri zaidi kesho.

Wanasoka sita ambao hawakucheza mechi dhidi ya Tusker kutokana na kuwa wagonjwa na maumivu mbalimbali ni Nicholas Meja, Abdalla Hassan, Yema Mwana, Fred Nkata, Danson Chetambe Namasaka na nahodha Felly Mulumba.

Hapo hapo, Mwalala alitoa wito kwa mashabiki wa timu yake wajitokeze kwa wingi kushangilia ili kuwapa moyo wachezaji wafanye bidii zaidi ya kupata ushindi. “Nawaomba mashabiki wetu wasizome bali washangilie,” akasema.

Alisema ana uhakika kukiweko na ushirikiano baina ya wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na mashabiki, matokeo mazuri yatapatikana na wapenzi wa soka wa Pwani watafurahikia. “Sina shaka Ijumaa kutakuwa na ushangiliaji mkubwa wa kuwezesha mashabiki kuhakikisha wanachezaji kwa ari na moyo wa ushindi,” akasema.