Mwalala: Ati! Shikalo? Hii Bandari FC itasumbua tu

KOCHA wa Bandari FC, Bernarda Mwalala aliyetuzwa kocha bora wa mwezi Mei/Juni kwenye tuzo za SJAK Fidelty Insurance Awards, kasisitiza kikosi chake kipo imara licha ya kumpoteza kipa smaku Farouk Shikalo.
Shikalo alikamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Yanga SC ya Tanzania siku chache zilizopita hatua ambayo wadau wa soka wamehoji imeiwacha pengo kubwa katika kikosi cha kocha Mwalala.
Hata hivyo, kulingana na kocha huyo, kikosi chake bado kipo imara kama Simba na ameahidi kitasumbua tena vibaya sana msimu mpya utakapoanza.
“Kikosi change kipo fiti bado sababu hakuna mchezaji mwingine niliyempoteza zaidi ya kipa Farouk Shikalo hivyo sio ishu kwani tayari tunaona watakaoziba nafasi yake” Mwalala alisema.
Huku akiendelea kukinoa kikosi chake kwa ajili ya dimba la CAF Confedarations, hofu yake kubwa ipo kwenye safu ya ushambuliaji anayosema bado ni butu na inahitaji kazi ya ziada.
“Mashindano ya Cecafa yalinipa fursa ya kujua ni idara ipi katika kikosi changu kinachohitaji maboresho na hiyo ni safu ya mashambulizi. Msimu wetu utakuwa bize sana kutokana na ushiriki wetu kwenye dimba letu la kwanza la CAF Confederation hivyo nitajitaji kuumiza kichwa kabisa kunyoosha mambo,” Mwalala aliongeza.
Mechi yao ya kwanza ya Caf Confederation itakuwa dhidi ya Al Alhy Shandy wa Sudan.  Ngoma hiyo itachezwa nyumbani Agosti 9, kabla ya mwanzo wa msimu wa ligi kuu ya KPL na baada ya wiki Bandari watasafiri hadi Sudan kwa ajili ya mchezo wa marudio.