Mwakyembe atoa mchongo kwa kampuni na taasisi

Muktasari:

Amesema kampuni na taasisi mbalimbali ambazo hazijajitokeza kwenye mashindano hayo yanapaswa kufanya hivyo kwa mwaka ujao kwasababu husaidia kujenga undugu pamoja na afya bora kwa wafanyakazi.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, amesema kampuni na taasisi mbalimbali nchini  zinapaswa kushiriki kwenye mashindano ya Shimuta yanayofanyika kila mwaka.

Mwakyembe amesema hayo leo Jumamosi jiji hapa kwenye Uwanja wa Nyamagana wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Shimuta 2019 akiwa ni Mgeni rasmi akimuwakilisha  Makamu wa Rais, Samia Suluhu.

Amesema kampuni na taasisi mbalimbali ambazo hazijajitokeza kwenye mashindano hayo yanapaswa kufanya hivyo kwa mwaka ujao kwasababu husaidia kujenga undugu pamoja na afya bora kwa wafanyakazi.

"Niwapongeze wenyeji wetu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuandaa mashindano haya kwa mwaka huu, Shimuta husaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa eneo husika pia wafanyakazi wakipata nafasi ya kushiriki hupelekea wawe na afya bora," amesema Mwakyembe.

Ameongeza, "Mwaka jana kulikuwa na timu 26 zilizoshiriki ambapo mashindano hayo yalifanyika jijini Dodoma, lakini kwa sasa zimeongezeka mpaka kufikia timu 46 hivyo kwa mwaka ujao, taasisi nyingine zinapaswa kushiriki,".

Pamoja na hayo, Waziri amezitaka kampuni kutumia wachezaji wafanyakazi tu na sio mamluki ili kuweka uhalisia wa mashindano hayo, pia amewaagiza waamuzi kuchezesha kwa haki na ambaye atashindwa kufanya hivyo basi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.