Waziri Mwakyembe ashika hatma ya Taifa Queens kushiriki mashindano Afrika

Muktasari:

Tangu mwaka 2013, Tanzania haijashiriki mashindano ya kimataifa ya netiboli hali iliyopelekea kufutwa uanachama kwenye Shirikisho la Afrika (ANF) na lile la dunia (IFNA) kabla ya kurejeshwa mwaka huu.

Dar es Salaam.Wakati timu ya Taifa ya Tanzania ya netiboli (Taifa Queens) ikiwa mguu ndani mguu nje kushiriki mashindano ya Afrika, mabosi wa Chaneta wanaendelea na kikao na Waziri wa Michezo Dk Harrison Mwakyembe kujua hatma ya timu hiyo.

Taifa Queens ni miongoni mwa timu nane za Afrika zinazotarajiwa kushiriki mashindano ya Afrika yatakayofunguliwa Ijumaa ijayo nchini Afrika Kusini.

Wachezaji 12, kocha na viongozi wawili wanayarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya siku tano yatashirikisha mabingwa wa Afrika, Afrika Kusini, Uganda na Malawi.

Hadi Leo Jumanne Oktoba 15, 2019, saa 8 Mchana timu ya Taifa haikuwa na uhakika wa kushiriki mashindano hayo kutokana na ukata huku viongozi wa Chaneta wakiendelea na kikao na Wizara ya Michezo mchana huu kujua hatma ya timu hiyo ambayo awali Serikali iliilipia dola 500 za ada ya ushiriki.

Katibu mkuu wa Chaneta, Judith Ilunda alisema wamekutana na waziri wa michezo, Dk Mwakyembe kujua hatma ya Taifa Queens na hadi kufikia saa 10 jioni Leo watatoa taarifa rasmi kama timu hiyo itakwenda Afrika Kusini au la.