Mwakyembe: Afcon hii imetufunza mengi

Muktasari:

Taifa Stars imemaliza fainali za Afcon ikiwa haijapata pointi yoyote baada ya kufungwa mechi zote tatu za Kundi C ikiwa pamoja na Algeria, Senegal na Kenya

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon2019) ni funzo kubwa kwa Tanzania.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuipokea timu ya Taifa Stars kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo Alhamisi Julai 4, 2019 ikitokea Misri.

Mwakyembe alisema matokeo na hata machakato mzima wa kufuzu Afcon umewafundisha mambo mengi ambayo watakwenda kuyafanyia kazi.

"Tumejifunza mengi ambayo baada ya kumaliza mashindano haya na timu kuwasili nchini leo, tutaanza maandalizi ya mashindano yajayo," alisema.

"Kuna mambo mengi kama maandalizi ya msingi ili timu kufuzu na hata ikifanikiwa iweze kufanya vizuri kwenye mashindano.

"Niwapongeze wachezaji wote wamecheza vizuri na wamepambana kwa nguvu zao zote ndio maana tulifuzu na tukacheza mashindano," alisema.

"Tutakutana kila ambaye anahusika na Taifa Stars ili kufanya yale mambo ya msingi ambayo tumejifunza katika mashindano ya msimu huu na kama itatokea msimu tukafuzu tufanye vizuri zaidi ya msimu huu," alisema mwakyembe.