Mwakinyo kuwania mataji mawili kwa mpigo

Bondia Hassan Mwakinyo atapanda ulingoni Novemba 13 kuzichapa kuwania mataji ya dunia ya WBF na wa mabara wa IBA.

Bondia huyo namba moja nchini kwenye uzani wa super welter atazichapa na Jose Carlos Paz wa Argentina pambano la raundi 12 .

Mkurugenzi wa Jackson Group, Kelvin Twissa amesema siku hiyo mabondia kutoka nchi tano watazichapa kumsindikiza Mwakinyo na Paz, akiwamo aliyekuwa bingwa wa dunia wa WBC, Fatuma Zarika kutoka Kenya.

Amesema Zarika atazichapa na Patience Mastara wa  Zimbabwe, na Zulfa Yusuph Macho atacheza na Alice Mbewe wa Zimbabwe.

"Dullah Mbabe 'Abdallah Pazi' atacheza na Alex Kabangu wa DR Congo," amesema Twissa.

Amesema pambano la Mwakinyo litakuwa la kutetea ubingwa wa WBF wa dunia alioshinda dhidi ya Tshibangu Kayembe wa DRCongo.

"Mapambano hayo yatapigwa kwenye ukumbi wa Next door Arena, Masaki, Dar es Salaam," amesema.

Katibu wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), Yahya Poli amesema Mwakinyo atazichapa kuwania ubingwa mwingine wa mabara wa IBA na wakati huo huo atatetea ubingwa wake wa dunia wa WBF.

Mwakilishi wa WBF nchini Tanzania,  Chatta Michael alisema pambano hilo litahudhuliwa na rais wa WBF, Goldberg Howard.

Akizungumzia maandalizi yake, Mwakinyo amesema yuko vizuri na amejipanga si tu kutetea ubingwa wa dunia, lakini pia kutwaa taji jingine la kimataifa.