Mwakinyo atua Kenya, kupima uzito kesho

Muktasari:

Kampuni ya SportPesa imeona umuhimu huo na lengo letu kubwa ni kuona mabondia hao wanapata matokeo mazuri na kuwafurahisha wadau wa ngumi za kulipwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Tarimba.

 Dar es Salaam. Bondia nyota wa Tanzania, Hassan Mwakinyo amewasili mjini, Nairobi Kenya tayari kwa pambano lake la Kimataifa dhidi ya bondia kutoka Argentina, Eduardo Gonzalez lililopangwa kufanyika Jumamosi kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (Kenyatta International Conference Centre).

Mwakinyo kwa sasa ananoa makali yake chini kocha Tony Bellew kutoka Liverpool, Uingereza ambako alikuwa kambini chini ya ufadhili wa Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa.

Mbali ya Mwakinyo, pia Bellew anamfundisha bondia Fatuma Zarika ambaye atapambana na Catherine Phiri wa Zambia katika pambamo la ubingwa wa dunia wa uzito wa Super Bantamweight wa Baraza la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBC).

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa Kampuni ya Sport Pesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema kuwa bondia Mwakinyo atafanya mazoezi chini ya kocha huyo chini ya uwezeshaji wa kampuni yao na wanatarajia kupata ushindi katika pambano lake.

Tarimba alisema kuwa mbali ya kampuni yao kuwezesha kambi ya Mwakinyo na Zarika, pia Bellew amevutiwa sana na viwango vya mabondia hao na wanaamini kuwa watafanya vizuri katika pambano hilo.

Alisema kuwa mabondia hao wamepata mafunzo bora na ya kisasa kutokana na umuhimu wa pambano hilo ambalo linatarajiwa kula kali na kusisimua. “Wakiwa mjini Liverpool, Mwakinyo na Zarika walijiandaa vyema kwa kuwa wanajua ugumu wa mapambano yao.

Kampuni ya SportPesa imeona umuhimu huo na lengo letu kubwa ni kuona mabondia hao wanapata matokeo mazuri na kuwafurahisha wadau wa ngumi za kulipwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Tarimba.

Alisema kuwa Gonzalez alitarajiwa kuwasili Kenya jana Jumarano kesho Ijumaa mabondia wote hao watapima uzito kwenye hotel ya The Stanley. Pia mabondia hao watatembelea ofisi za SportPesa na kufanya mahojiano kwenye vituo mbalimbali vya televisheni na redio mbali ya kula chakula cha jioni na wafanyakazi wa kampuni yao.