Mwakinyo atinga bungeni, alamba 20, za wabunge

Muktasari:

Bondia huyo kwa mara ya kwanza ameshinda katika pambano lake alilocheza nje ya Tanzania

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo leo Ijumaa amekaribishwa na kutambuliswa Bungeni kwa makofi na vifijo huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akipitisha azimio la wabunge wote waliohudhuria mkutano wa Bunge kumchangia sh20, 000 kila mmoja.

Mwakinyo amepata umaarufu Duniani baada ya kumchapa bondia Muingereza Sam Eggington kwa Technical Knock Out (TKO)

Baada ya Bondia huyo kuwasili bungeni majira ya saa 11:34 asubuhi, Spika wa Bunge Ndugai alimtambulisha na wabunge wote kupiga makofi na vifijo.

Ndugai alisema "tunakupongeza na tunaona fahari kuwa mwenzetu na umeliletea Taifa heshima kubwa.

"Ni matarajio yetu sasa hivi utasonga mbele, mbele zaidi na naomba tutakapomaliza hapa Mwakinyo apelekwe kuonana na waziri mkuu popote alipo," alisema Ndugai na kushangiliwa kwa makofi.

Hata hivyo baadae Spika alitania "Sikujua kama Tanga mtatoa Bondia, nilijua bondia atatoka usukumani, kwa wanyamwezi wabeba mizigo mizito kumbe hakuna chochote," jambo lililofanya wabunge kuangua vicheko.

Baada ya kusema hayo, Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hillaly aliomba mwongozo na kusema" Tumekuwa tukiwachangangia mamiss humu ndani, tunaomba mwongozo wako sisi kama wabunge tumchangie hata elfu 20 na kufanya wabunge kupiga makofi.

Spika Ndugai alisema nafikiri kwa makofu hayo tumeafikiana.