Mwaisabula: Simba watulie, wasisajili kwa mihemko

Muktasari:

  • Mwaisabula anasema ammefanya tathmini kikosi cha Simba na kubaini kuwa uongozi wa timu hiyo hauna haja ya kufanya usajili mkubwa kama watani zao Yanga kwani mahitaji ya timu zao zilikuwa tofauti.

KOCHA wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa masula ya soka Kennedy Mwaisabula amewataka viongozi wa Simba kutuliza akili kipindi hiki cha usajili ili kupata wachezaji bora ambao wataisaidia timu yao msimu ujao.
Mwaisabula anasema ammefanya tathmini kikosi cha Simba na kubaini kuwa uongozi wa timu hiyo hauna haja ya kufanya usajili mkubwa kama watani zao Yanga kwani mahitaji ya timu zao zilikuwa tofauti.
“Ukiangalia kikosi cha Simba hata katika mashindano yote ya hapa ndani walikuwa imara na hakukuwa na timu ambayo ilionesha ushindani kwani maeneo mengi walikuwa bora na imara,”
“Simba wanatakiwa kuwa watulivu na kuangalia mapungufu machache waliyayofanya msimu uliopita hasa Ligi ya Mabingwa Afrika na sio kusajili kwa mihemko.
“Yanga wao wanavyofanya ni sawa kwani timu yao msimu uliopita wachezaji wengi walicheza lakini walikuwa na viwango vya kawaida na ndio maana uongozi mpya ulifanya tathmini na kubaini wanatakiwa kusajili wachezaji wasiopungua 11, jambo ambalo naungana nao,” anasema Mwaisabula.