Mwadui yaifuata Yanga, macho kwa Ajibu

Muktasari:

  • Mwadui inawakabili Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao uliopita ikiwa uwanja wake wa nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya Singida United.

Mwanza. Mwadui FC itashuka uwanjani kesho Jumanne kuwakabili vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga huku akili yao yote kwa Ibrahimu Ajibu.

Yanga inayoongozwa Kocha Mwinyi Zahera haijapoteza mchezo wowote msimu huu na kuongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 50.

Pamoja na rekodi hiyo ya Yanga, lakini wachezaji Mwadui FC wanasema kazi yao itakuwa ni kuifunga Yanga na kuvunja rekodi waliyonayo ya kutopoteza mchezo wowote kwenye Ligi Kuu.

Beki wa Mwadui, Revocatus Mgunga alisema kutokana na majukumu aliyopewa atayatekeleza vyema kuhakikisha mshambuliaji Ajibu hafurukuti katika lango lao wala kupenyeza mipira yoyote.

Alisema kuwa licha ya Heritier Makambo kuongoza kufunga mabao, lakini haoni kama nyota huyo ana madhara yoyote kama Ajibu, hivyo atakuwa makini naye sana.

“Achana na Makambo sijui Ngassa wala Fei Toto, mtu mbaya pale ni Ajibu, kwahiyo akili zangu zitakuwa kwake kuhakikisha hapenyezi mipira yoyote, najiamini katika ulinzi”alisema Beki huyo aliyemzingua John Bocco wa Simba.

Naye mshambuliaji wa klabu hiyo, Salim Aiyee alisema kazi yake ni kufunga mabao na kwamba kasi yake anataka kuionyesha zaidi katika mchezo huo ili kujiweka nafasi nzuri ya kuwania kiatu cha mfungaji bora.

 “Mimi kazi yangu ni kufunga mabao tu, najua haitakuwa rahisi kwa sababu Yanga ni timu kubwa na wazoefu kwenye Ligi lakini najua mbinu nitakazotumia kuwapita mabeki wake,”alisema Aiyee mwenye mabao nane hadi sasa.

Kocha wa timu hiyo, Ally Bizimungu alisema tayari ameshatoa majukumu kwa kila mchezaji wake, hivyo wanasubiri muda ili kuona nini kitajiri, huku akisisitiza kuwa pointi tatu ni muhimu.