Mwadui FC yawaonyesha njia wasugua benchi

Sunday June 24 2018

 

By SADDAM SADICK

KIMENUKA unaambiwa. Uongozi wa Klabu ya Mwadui umetangaza kuwafungulia milango ya kutokea wachezaji ambao walicheza chini ya kiwango na wale waliokosa namba msimu uliopita.
Katibu Mkuu wa timu hiyo,Ramadhan Kilao alisema kuwa msimu ujao wanahitaji kuwa na kikosi imara,hivyo wachezaji ambao hawakuonyesha kiwango msimu uliopita hawana nafasi kwao.
Alisema kuwa mbali na waliocheza chini ya kiwango,Klabu itaangalia pia waliokosa namba na waliocheza mechi chache kuhakikisha wanaondoka kwani ni kama mizigo.
“Lazima tuache hilo halina ubishi,lakini tutakaowaacha ni wale waliocheza chini ya kiwango,waliokosa namba na waliocheza mechi chache,msimu ujao tunataka kumaliza Ligi tukiwa nafasi nne za juu”alisema Kilao.
Katibu huyo aliongeza kuwa wanaendelea kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji ambao walivutiwa na Benchi la Ufundi kuhakikisha wanakuwa nao pamoja na kumpata Kocha Msaidizi.
Alisema kuwa msimu ujao Ligi itakuwa na ushindani mkali kutokana na kuongezeka kwa timu,hivyo lazima wajipange na kwamba bado Kocha wao Mkuu,Ally Bizimungu ni mali yao.
“Wapo wachezaji tuliovutiwa nao kwenye timu zao na mazungumzo yanaendelea sambamba na kwa Kocha Msaidizi,kiufupi tunaendelea kujipanga kwa ajili ya msimu ujao”alisema Kiongozi huyo.
Kilao alifafanua kuwa baada ya wiki moja ndio watatangaza rasmi wachezaji waliotemwa na walioingia na kwamba zoezi zima litasimamiwa na Kocha Bizimungu.

Advertisement