Mwadui FC yashusha vifaa kutoka nje

Muktasari:

  • Kocha mkuu wa klabu hiyo, Ally Bizimungu alisema kutokana na mahitaji yao wameamua kuwashusha nchini nyota wawili kutoka Ghana na Uganda ili kuzipa changamoto timu pinzani na kumaliza ligi kwenye nafasi nzuri.

ZIKIWA zimebaki siku chache kabla dirisha dogo la usajili kufungwa, Mwadui imefanikiwa kunasa silaha mbili na kuzisainisha kandarasi ya mwaka mmoja kila mmoja.

Timu hiyo ambayo imetoka kuvuna ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Alliance inaendelea kujiimarisha kuhakikisha inafanya vizuri kutokana na kutoanza vyema msimu huu.

Kocha mkuu wa klabu hiyo, Ally Bizimungu alisema kutokana na mahitaji yao wameamua kuwashusha nchini nyota wawili kutoka Ghana na Uganda ili kuzipa changamoto timu pinzani na kumaliza ligi kwenye nafasi nzuri.

Aliwataja nyota hao kuwa ni kiungo mshambuliaji, Evans Sekazza (Uganda) na straika, Soa Benjamin raia wa Ghana.

“Ni mapendekezo ya benchi la ufundi kuhitaji timu ifanye vizuri, tunachotaka ni kuona Mwadui inashinda kila mchezo kwa mabao mengi, tunaamini ujio wa nyota hawa utaleta mabadiliko makubwa,” alisema Bizimungu.

Kocha huyo aliongeza baada ya kukamilisha dili hilo la nyota wa kimataifa, kwa sasa wanaumiza kichwa kumalizana na wachezaji wengine wawili ili kukiweka kikosi fiti tayari kwa kuanza kazi.

Alisisitiza kwa mwenendo walionao hivi sasa haoni timu itakayopenya miguuni mwao bila kuonja kipigo kutokana na maandalizi yao.