Mwadui: Hatuwaogopi Simba

MSHAMBULIAJI wa Mwadui FC, Pastory Athanas amesema licha ya Simba kupoteza michezo miwili mfululizo haitawafanya waidharau kwani itabaki kuwa Simba tu.

Mwadui itakuwa Dar es Salaam leo Jumamosi kucheza na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Simba imekuwa ikipata ushindi dhidi ya Mwadui mara nyingi iwe Dar es Salaam au ugenini kwani kwa msimu mitatu mfululizo Wekundu wa Msimbazi wameshinda mechi zote tatu walizokutana na Mwadui jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo uliofanyika Septemba 17, 2017 Simba iliifunga Mwadui kwa mabao 3-0 kisha ikapata ushindi kama huo Februari 7, 2018 na tena mabao 3-0 Juni 20, mwaka huu.

Hata hivyo, Mwadui inaweza kutumia fursa ya Simba kupoteza mechi mbili mfululizo kama njia ya kupata ushindi kwani ndani ya Wekundu wa Msimbazi hivi sasa kunafukuta baada ya kupokea vipigo mfululizo kwa bao 1-0 dhidi ya Prisons na Ruvu Shooting jambo lililosababisha kumtimua meneja Patrick Rweyemamu na kocha wa makipa, Mohammed Mharami.

Jambo hilo ndilo limempa hofu Athanas ambaye amekiri wanatakiwa kuikabili Simba kwa tahadhari kubwa kwani inaweza kuingia uwanjani tofauti.

“Tumejiandaa vizuri na mechi hiyo, lakini nikiri itakuwa ngumu sana kwani wapinzani wetu huko kwao mambo hayapo vizuri, lakini tutapambana kujaribu kupata matokeo katika dakika 90,” alisema Athanas.

“Wamepoteza mechi mbili mfululizo, lakini hilo halitufanyi tuwakabili kwa kuwadharau kwa sababu Simba watabaki kuwa Simba - maana wana wachezaji wazuri waliokaa pamoja muda mrefu, hivyo wanaweza kufanya lolote na wakapata matokeo. Sio kwamba tunawahofia, hapana ila tunawaheshimu kwani wana timu nzuri iliyo na wachezaji wengi wa kigeni.”