Mvuto usiokwisha wa Ligi Kuu England

Muktasari:

  • Upinzani uliopo kwenye ligi hiyo unaleta mambo yanayovutia ikiwamo haya sita yaliyopatikana baada ya mechi zilizochezwa wikiendi hii iliyopita.

LONDON, ENGLAND. LIGI Kuu England imekuwa ikihesabika kama moja ya ligi bora kabisa duniani kwa sasa kutokana na upinzani uliopo kwenye mikikimikiki hiyo.

Upinzani uliopo kwenye ligi hiyo unaleta mambo yanayovutia ikiwamo haya sita yaliyopatikana baada ya mechi zilizochezwa wikiendi hii iliyopita.

6. Arsenal yakomaa na timu za Top Six msimu huu

Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, Arsenal imevuna pointi 12 katika mechi 10 ilizocheza dhidi ya wababe wenzake wa Top Six kwenye ligi hiyo kwa msimu huu.

Pointi hizo 12 ni mara mbili ya kile ilichovuna msimu uliopita ambapo kwenye mechi za Top Six iliambuliwa pointi sita tu. Msimu huu wameonekana kuwa moto zaidi na kugoma kupoteza pointi ovyo wakiwa chini ya kocha Unai Emery.

5. Aubameyang anazidiwa na Salah na Aguero tu

Tangu alipoanza kucheza kwenye Ligi Kuu England mechi yake ya kwanza Februari 2018, straika wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang amefunga mabao 18 katika mechi zilizochezwa kwenye uwanja wa nyumbani.

Kwa mabao hayo, staa huyo wa kimataifa wa Gabon anazidiwa na Mohamed Salah wa Liverpool (mabao 20) na Sergio Aguero wa Manchester City (mabao 19) kwa kufunga mara nyingi kwenye mechi za nyumbani kwa kipindi hicho cha kuanzia Februari mwaka jana hadi sasa.

4. Arsenal ikicheza na Man United Jumapili, inashinda

Kama kuna kitu ambacho Arsenal ilikuwa ikifurahia kwelikweli kwenye mechi yao dhidi ya Manchester United basi kuchezwa Jumapili.

Mara nyingi, Arsenal ilipomenyana na Man United Jumapili, basi wamekuwa wakiibuka na ushindi. Juzi Jumapili, walifanya hivyo tena waliposhinda 2-0, shukrani kwa mabao ya Granit Xhaka na Pierre-Emerick Aubameyang.

Rekodi zinaonyesha kwamba Arsenal imeichapa Man United 14 kwenye Ligi Kuu England na mara 10 ni kwenye mechi zilizochezwa Jumapili.

3. Hazard akaa pamoja na akina Drogba

Eden Hazard amekuwa mchezaji wa tatu wa Chelsea baada ya Frank Lampard na Didier Drogba kwa kufikisha mabao 50 au zaidi ya Ligi Kuu England uwanjani Stamford Bridge.

Manchester United peke yao ndiyo yenye wachezaji wengi, watano waliofikisha mabao 50 au zaidi kwenye Ligi Kuu England katika mechi zao walizocheza uwanja wa nyumbani, Old Trafford.

2. Firmino mchezaji muhimu zaidi Liverpool

Kwenye kikosi cha Liverpool, Roberto Firmino ndiye mchezaji muhimu zaidi katika timu hiyo kutokana na kuwa na mchango wake usiokuwa na kikomo.

Mbrazili huyo amefunga mabao 10 na zaidi kwa misimu minne aliyochezea Liverpool kwenye Ligi Kuu England na hivyo kuwa mtumishi muhimu kabisa kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Anfield.

1. Sterling akifunga, Man City inashinda

Staa, Raheem Sterling ameibuka kwenye upande wa timu ya ushindi mara zote 34 ambazo yeye alifunga bao.

Jambo hilo linafanya kuwa na rekodi tamu na kwamba Sterling amekuwa na bahati kwenye kikosi hicho kwa sababu kila anapofunga bao, basi ujue siku hiyo, mabingwa hao watetezi wa England wanashinda mechi hiyo.